RC Macha awataka wananchi wajitokeze kujiandikisha daftari la wakazi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 08:33 PM Oct 08 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza wakati wa kuzindua zoezi uandikishaji daftari la mpiga kura.
Picha:Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza wakati wa kuzindua zoezi uandikishaji daftari la mpiga kura.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amewataka Wakazi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wakazi kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 huku akihamasisha wananchi wote wanawake kwa wanaume wenye sifa kuchukua fomu ili kuwania nafasi za uongozi ngazi ya mtaa, kijiji na kitongoji.

Macha ametoa rai hiyo leo Oktoba 8,2024 wakati wa Uzinduzi wa Zoezi la Uandikishaji wa Daftari la Wakazi kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga litakaloanza Oktoba 11,2024 hadi 20 likiongozwa na Kauli mbiu "Serikali za mitaa, sauti ya wananchi, jitokeze kushiriki uchaguzi".

"Akina mama wamechangamka sana safari hii, tuhakikishe tunapata uongozi wa pamoja hivyo niwaombe wanaume kwa wanawake tujitokeze kugombea nafasi za uongozi kwa sababu uchaguzi utafanyika ukizingatia makundi yote ya watu katika jamii. Tunawatia moyo watu wote wajitokeze kugombea nafasi za uongozi wanaojua kusoma na kuandika wenye umri kuanzia miaka 21, mwenye akili timamu ,raia wa Tanzania,",amesema Macha.

Amesema Uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 katika Mkoa wa Shinyanga utafanyika katika mitaa 90, vitongoji 2,704 na vijiji 506.

Aidha Macha amewataka wananchi wachague viongozi bora ambao watawaletea maendeleo.

"Tuwachague viongozi bora, watakao tuletea maendeleo, niwapongeze viongozi wa serikali za mnaomaliza muda wenu lakini mnaruhusiwa kugombea tena wananchi ndiyo wataamua",amesema Macha.

Hata hivyo amesema uchaguzi utakuwa wa huru na haki na serikali imejipanga vizuri kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga ,Elias Ramadhan Masumbuko amewataka wananchi kutumia vizuri muda wa kujiandikisha kila mmoja ajiandikishe kwani suala hilo linafanyika kwa misingi ya haki na amani.

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Charles Kafutila amesema halmashauri hiyo ina kata 17, vijiji 17, vitongoji 84 na mitaa 55 na zoezi la uandikishaji wapiga litafanyika katika vituo 199 ambapo lengo la Halmashauri ni kuandikisha wapiga kura 120,345.