Dk. Yonazi: Serikali imeweka mifumo kuimarisha usimamizi wa maafa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:00 PM Oct 08 2024
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi.
Picha:Mpigapicha Wetu
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi amesema serikali imeweka mfumo wa kisera, kisheria na kitaasisi kwa lengo la kuendelea kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa nchini.

Akizungumza leo Wilayani Hanang mkoani Manyara, Dk. Yonazi amesema mifumo hiyo inaenda sambamba na kutunga sera ya taifa ya menejimenti ya maafa ya mwaka 2004 na sheria ya usimamizi wa maafa, namba sita ya mwaka 2022, ambayo imebainisha majukumu na kuweka mfumo wa usimamizi wa maafa kupitia kamati za usimamizi wa maafa kutoka ngazi ya taifa kijiji, na mtaa. 

Amesema lengo la hatua hizo ni kuhakikisha wizara, idara, taasisi za serikali na zisizo za serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, zinashiriki kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali kwa ubora pindi maafa yanapotokea. 

"Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, itaendelea kuimarisha masuala ya menejimenti ya maafa kwa lengo la kuimarisha ustahimilivu dhidi ya maafa nchini," amesema na kuongeza:

"Ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa kwa ufanisi, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na wadau, imeendelea kuboresha utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa majanga kwa kuandaa nyaraka zinazoainisha majukumu ya msingi na mwongozo kwa wadau," amesema Dk. Yonazi.

Aidha, ameeleza kuwa nyaraka hizo ni pamoja na mpango wa taifa wa kujiandaa na kukabiliana na maafa, mkakati wa taifa wa mawasiliano wakati wa maafa, na mkakati wa taifa wa usimamizi wa maafa wa 2022.

Dk.Yonazi amesema nyaraka hizo ziwe ni chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau pamoja na  kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa na kukabiliana na maafa.

“Natambua, kwa sasa halmashauri inaendelea kutekeleza shughuli za kurejesha hali baada ya maafa makubwa yaliyosababishwa na janga la maporomoko ya ardhi katika mlima Hanang yaliyotokea mwaka jana.

"Niendelee kusisitiza kuwa, muendelee  kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa na kukabiliana na maafa na kuwahamasisha wananchi kutokutekeleza shughuli za kiuchumi na ujenzi katika maeneo hatarishi kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu,” amesema Dk. Yonazi.