MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amesema wanafunzi wakike wanahitaji faragha ya kujistiri hedhi,pale wanapokuwa katika mazingira ya shule ili kulinda utu wao.
Amebainisha hayo leo Octoba 3,2024 wakati Taasisi ya Flaviana Matata Foundation, ilipokuwa ikikabidhi choo cha kisasa chenye matundu 12 kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Masekelo manispaa ya Shinyanga, kikiwa na chumba maalumu cha kujistiri hedhi.
Amesema anaipongeza taasisi hiyo kwa kusaidia wanafunzi wa kike kukuza taaluma zao, kwa kuwajengea choo chenye chumba maalumu cha kujistiri hedhi ili wasikose vipindi vya masomo wanapokuwa katika siku zao, na kwamba suala hilo lina hitaji faragha.
“Mwanafunzi wa kike anahitaji faragha kujistiri hedhi, na huo ndiyo utamaduni na heshima ya binadamu kwa kulinda utu wao, na hata kuzihifadhi taulo za kike ambazo zimetumika na zenyewe ni faragha, ndiyo maana katika choo hiki cha Flaviana kuna kichomea taka,”amesema Macha.
Aidha, amempongeza Flaviana kwa Taasisi yake hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza sekta ya elimu, kwa kujenga vyoo vya kisasa kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule mbalimbali mkoani humo, kufadhili masomo wanafunzi pamoja na kuwapatia taulo za kike kila mwezi ili wasikose vipindi vya masomo.
Mkurugenzi Mtendaji Taasisi hiyo Flaviana Matata, amesema wamekuwa wakiunga mkono sekta ya elimu kwa wanafunzi wa kike, na katika Mkoa wa Shinyanga wamekuwa na mradi wa ujenzi wa vyoo vya wasichana vyenye chumba maalumu cha kujistiri hedhi, pamoja na kuwafadhili masomo na kuwapatia taulo za kike kila mwezi.
Amesema katika shule hiyo ya Sekondari Masekelo, wamejenga choo cha wasichana chenye matundu 12 kikiwa na chumba maalumu cha kujistiri hedhi pamoja na kichomea taka, na wanawafadhili wanafunzi watano kimasomo, na kwamba kila mwezi hua wanawapatia wasichana 30 taulo za kike katika shule hiyo.
Mkuu wa shule ya Sekondari Masekelo Vicent Kanyogota, amesema upatikaji wa chumba maalumu cha wanafunzi wa kike kujistiri hedhi shuleni hapo, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoro, na hata kufanya vizuri kitaaluma sababu hawatakuwa wakikosa vipindi vya masomo tena.
Nao wanafunzi wa kike katika shule hiyo akiwamo Ester Jackson, ameipongeza taasisi hiyo, kwamba hawatakuwa wanakosa vipindi tena vya masomo, sababu wanachumba cha kujistiri hedhi na watafanya vizuri kitaaluma.
Ujenzi wa choo hicho cha wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Masekelo, umetekelezwa na Taasisi ya Flaviana Matata kwa ufadhili wa Diamond Do Good.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED