Rais Samia asherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika na wajukuu

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:32 AM Jun 17 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akisherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika akiwa pamoja na wajukuu, Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Siku hii huadhimishwa Juni 16 ya kila mwaka.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan akisherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika akiwa pamoja na wajukuu, Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Siku hii huadhimishwa Juni 16 ya kila mwaka.

RAIS Samia Suluhu Hassan ameadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kualika watoto kutoka sehemu mbalimbali nchini kisha kusherehekea nao kwa michezo, kuchora na kutembelea Ikulu ya jijini Dar es Salaam.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 kila mwaka. Kwa Tanzania kaulimbiu ni ‘Elimu Jumuishi kwa Watoto Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi’. 

Lengo la maadhimisho hayo ni kukumbusha juhudi zinazofanywa kunyanyua mtoto wa Afrika na changamoto zinazotokea katika kuhakikisha anapata elimu bora. 

Katika kuadhimisha siku hiyo jana, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa serikali, familia na jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yenye maadili mema.

Rais Samia alihimiza kuhakikisha usalama wa mtoto unakuwa jukumu la jamii nzima na siyo mzazi tu, pia akasisitiza kuwapatia elimu na historia za kuwahimiza uzalendo kwa nchi yao tangu wakiwa wadogo.

 Watoto hao walipata muda wa kujifunza mambo mbalimbali kuhusu nchi yao pamoja na kuburudika na michezo ya aina tofauti.

 Video fupi iliyowekwa katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram wa Ikulu, ilimwonyesha Rais Samia akiwaongoza watoto hao kuchora picha ya Bendera ya Taifa huku akiwatia moyo na kuwapa motisha.

 Rais pia alifundisha watoto kuhusu Ikulu kwa kuwauliza maswali ili kujua ufahamu wao kuhusu ofisi hiyo kuu nchini kisha kuwaelekeza pale alipoona wanahitaji ufafanuzi.

“Hapa ni wapi? Ikulu au Posta? Ikulu anakaa nani?  Ikulu hakai Mama Samia wala Bibi Samia, Ikulu anakaa Rais,” alisema.

 Baada ya kumaliza shughuli za nje, Rais aliwapeleka ndani ya jengo la Ikulu na kuwatembeza sehemu mbalimbali, ikiwamo ofisini kwake.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, alimshukuru Rais Samia kwa kutenga muda wake kusherehekea na watoto na kuhimiza wazazi kujenga utaratibu wa kutenga muda wa kukaa, kuzungumza na kucheza na watoto wao.

 Kupitia ukurasa wake wa Instagram, waziri huyo aliandika, “Shukrani Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga muda wako na watoto kwenye Siku hii ya Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika.”