Pwani wapokea wawekezaji 23 kutoka China, matunda ziara ya Rais Samia

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:36 PM Nov 08 2024
 Pwani wapokea wawekezaji 23 kutoka China, matunda ziara ya Rais Samia
Picha:Mpigapicha Wetu
Pwani wapokea wawekezaji 23 kutoka China, matunda ziara ya Rais Samia

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa ziara alizofanya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika nchi mbalimbali duniani zimeanza kuleta mafanikio katika mkoa huo baada ya kuanza kupokea wageni wanaotaka kuwekeza.

Kunenge amesema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mara  baada ya kikao kifupi na wageni 23  kutoka Jimbo la Jilin lililopo nchini China ambao wametembelea mkoa huo.

Kunenge, amesema lengo la ziara ya wageni  hao kutoka China ni kuangalia fursa za maeneo ya uwekezaji ikiwa ni baada ya kushawishika na uhamasishaji uliofanywa na Rais Samia alipokwenda nchini kwao na kukutana na Rais wa China hivi karibuni.

Kunenge amesema kuwa katika kikao hicho cha pamoja  wamekubaliana kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ya uwekezaji ambapo kutakuwa na mkataba maalum wa makubaliano kwenye uwekezaji wa maeneo yatakayowekezwa.

"Kabla ya kuja hapa nchini na katika Mkoa wetu walifanya utafiti na kubaini Pwani ni Mkoa unaoongoza kwa uwekezaji wa viwanda, tumewaambia tunachotaka ni kuwa na uwekezaji wenye tija na sisi tutajifunza kutoka kwao," amesema Kunenge 

Mkuu huyo wa Mkoa amesema mbali ya ukaribisho uliofanywa na Rais Samia pia sera za nchi ni moja ya vitu vilivyowavutia raia hao kuja nchini kwa ajili ya kufanya uwekezaji.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa kamati ya watu wa Jimbo la Jilin lililopo nchini China ambaye pia ndiye kiongozi wa msafara huo  Gao Guangbin, amesema kuwa ujio wao Mkoa wa Pwani umetokana na ushirikiano wa nchi mbili ikiwemo Tanzania na China 

Guangbin, amesema kuwa Rais wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amekuwa Rais mwenye kuendeleza ushirikiano kwa kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika nchi yake jambo lililowapa msukumo wa kufika hapa nchini kuangalia fursa zilizopo.

Amesema, ziara yao kwa Mkoa wa Pwani haikuwa bahati mbaya kwani kwa muda mrefu kumekuwa na wawekezaji wengi kutoka China ambao wanafanya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika Mkoa wa Pwani ambao umekuwa na fursa nyingi za uwekezaji.

Ameongeza kuwa,pamoja na mambo mengine China inaushirikiano mkubwa na Afrika na Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikishirikiana kwa ukaribu na China katika kufanya uwekezaji mbalimbali.

Awali Katibu Tawala Msaidizi wa uchumi na Uzalishaji Shangwe Twammala,amewaambia wagenj  hao kuwa Mkoa wa Pwani bado kuna ardhi ya kutosha na inayofaa kwa uwekezaji katika  nyanya mbalimbali ikiwemo ujenzu wa viwanda,Uvuvi,Kilimo,Utalii na Sekta nyingine.

Twammala amesema kuwa kwa upande wa viwanda Mkoa wa Pwani umekuwa ukiongoza ambapo mpaka kufikia Machi mwaka huu Mkoa ulikuwa na viwanda 1,535 vilivyosaidia kutoa ajira za kudumu na muda mfupi zaidi ya 18000.

Kikao cha pamoja na wageni hao kimehudhuriwa pia na  Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta,sekretarieti ya Mkoa,baadhi ya Wakuu wa taasisi za Serikali ikiwemo Ruwasa na Tanroads.