MWANAFUNZI wa Darasa la tatu katika Shule ya Msingi Luchelele iliyopo jijini Mwanza, Kurwa Mkami (9) amefariki dunia baada ya kushambuliwa kisha kuvutwa kwenye maji na mamba wakati akioga kwenye fukwe za Ziwa Victoria.
Tukio hilo limetokea Novemba 5, 2024 majira ya saa 12 jioni katika mwalo wa Ihumilo, Kata ya Luchelele jijini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilibroad Mutafungwa leo Novemba 8,2024.
DCP Mutafungwa amesema baada ya kupokea taarifa hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori (TAWA) na Wananchi wa eneo hilo walifika katika mwalo huo na kuanza jitihada za kumtafuta Kurwa.
Amesema ilipofika Novemba 7, 2024 waliupata mwili wa marehemu ukiwa na majeraha ya kujerehiwa na mamba sehemu mbalimbali hali iliyosababisha umauti wake.
"Mwili wa marehemu Kurwa Mkami umefanyiwa uchunguzi wa kitaalam na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi. Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza pamoja na kutoa elimu pia linawaasa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya fukwe za ziwa Victoria kuchukuwa tahadhari za kiusalama wakati wanafanya shughuli zao kwenye fukwe za ziwa hilo ili kuepuka kushambuliwa na wanyama wakali," amesema DCP Mutafungwa.
Kufuatia tukio hilo TAWA alifanya oparesheni na kumuua kipoko kisha kumjeruhi Mamba huyo ambaye mpaka sasa anatafutwa ili kuondoa taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.
Ofisa Mfawidhi kutoka TAWA kituo cha Mwanza Godfrey Baisa amesema kutokana na mamba huyo kujeruhiwa wanauhakika wa kumpata muda wowote na kuwa oparesheni hiyo itakuwa endelevu kudhibiti wanyama wanaohatarisha maisha ya wananchi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED