Mshtuko CCM kumchangia Lissu

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:14 AM Aug 17 2024
Mshtuko CCM kumchangia Lissu.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mshtuko CCM kumchangia Lissu.

UAMUZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumchangia fedha Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu anunue gari jipya, umeibua minong'ono:

Wachambuzi wa siasa wamesema mwitikio wa Watanzania wengi kumchangia mwanasiasa huyo wa upinzani umeishtua CCM na kuona kuna haja wao pia wamchangie fedha; kufanya hivyo ni fursa kwao kisiasa. 

Kwa upande wa chama chake - CHADEMA, viongozi wanavuta subira, wakisisitiza kauli itatolewa baada ya kujiridhisha "kweli CCM wameweka fedha katika akaunti ya Lissu".   

Agosti 14 mwaka huu, Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, aliendesha harambee ya kumchangia fedha Lissu ili atengeneze gari lake ambalo alikabidhiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma Mei 17, mwaka huu. 

Ni gari lenye matobo ya risasi za tukio la kushambuliwa kwa silaha za moto Septemba 7, 2017, wakati anajiandaa kushuka nyumbani kwake Area D, jijini Dodoma. 

Harambee hiyo ilifanyika kwenye Uwanja wa Furahisha, jijini Mwanza wakati wa mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, Sh. milioni 5.3 zikichangwa. 

Mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza, alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia uamuzi huo wa CCM, alisema michango ya kununua gari la Lissu haikuanzishwa na Lissu, bali Watanzania wanaompenda ambao walikubaliana anunue gari jipya badala ya kutengeneza lile lililoshapigwa risasi. 

"Wapenzi wake wakaona gari lile liwe historia. Ninachokiona ni kwamba, mwitikio wa watu wanaomuunga mkono Lissu ndio ulioisukuma CCM kumchangia. CCM wameona ni jambo la kisiasa. Katika hali ya kawaida ni jambo zuri," alisema. 

Kaiza alisema mchango huo umeipa CCM fursa ya kuwapa wanachama wake wenye mapenzi mema kumchangia kiongozi huyo ambaye ni kada wa CHADEMA. 

Mchambuzi wa siasa, Luwaga Kizoka, alisema uamuzi huo wa CCM umeonesha ukomavu wa kisiasa, akisisitiza wanasiasa wanapaswa kupingana kiitikadi na si kujenga uadui. 

"Ni hatua nzuri ambazo uongozi wa juu wa chama (CCM) unaendelea kuzichukua kuhakikisha kwamba siasa za maridhiano na kujenga upya zinapewa kipaumbele katika awamu ya sita (Falsafa ya R4 za Rais Samia Suluhu Hassan)," alisema Kizoka. 

KAULI CHADEMA

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje CHADEMA, John Mrema, alipotafutwa na Nipashe jana kutaka kujua msimamo wa chama chao baada ya harambee hiyo ya CCM kufanyika, alisema hawawezi kutoa kauli kwa sasa. 

Mrema alisema, "hatuwezi kutoa kauli kwa sasa kwa sababu hatujathibitisha kama fedha hizo zimeingizwa kweli katika akaunti ya Makamu Mwenyekiti (Lissu) au la". 

Katika mkutano wa CCM ulioendesha harambee kumchangia Lissu, Makalla alisema amesikitishwa na taarifa iliyotolewa na kada wa zamani wa CHADEMA, Mch. Peter Msigwa, kada mpya wa CCM, kwamba, wakati kiongozi wake akipaa na chopa angani na msafara wa magari 15, Lissu amekuwa akitumia gari moja bovu na walinzi wake licha ya hali aliyonayo kiafya. 

Makalla alisema Lissu ni ndugu yake na wanatoka mkoa mmoja wa Singida na kuomba walioguswa kumchangia ili gari hilo litengenezwe. Katika harambee hiyo, baadhi ya makada wa CCM, akiwamo Katibu Mkuu Balozi Nchimbi, walichangia na kupata kwa kiasi hicho - Sh. milioni 5.3. 

Akizungumza na chombo kimoja cha habari, si Nipashe, Lissu alisema jana kuwa, "Ninawashukuru. Kama nilivyosema, hao waliosema wananichangia, hatukusema ni wana-CHADEMA peke yao, kama nilivyotibiwa, sikutibiwa na wana-CHADEMA peke yao, (CCM) wakichanga nitazipokea, sina sababu ya kukataa." 

*Imeandaliwa na Romana Mallya na Restuta James