MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma imetupilia mbali malalamiko yaliyofunguliwa na Wakili Paul Kisabo dhidi ya Fatma Kigondo, maarufu kama Afande, kutokana na dosari mbalimbali zikiwamo kutofuata utaratibu, hivyo kukosa sifa ya kutiwa saini kuwa hati ya mashtaka.
Oktoba 15, mwaka huu, wakili wa mlalamikaji, Peter Madeleka, alimwomba Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Nyambuli Tungaraja, kutia saini malalamiko hayo ili yatumike kama hati ya mashtaka na mshtakiwa asomewe popote alipo ili hatua zingine za kisheria ziendelee.
Akisoma uamuzi wa mahakama hiyo jana kuhusu maombi hayo ya Wakili Madeleka, Hakimu Tungaraja, alisema, mahakama imetupilia mbali malalamiko hayo yaliyofunguliwa na Kisabo dhidi ya Fatma kutokana na kasoro mbalimbali.
Hakimu huyo alisema malalamiko hayo yamekosa sifa ya kuwa hati ya mashtaka kutokana na kutofuata utaratibu wa uandaaji na uwasilishaji.
Alisema moja ya kasoro hizo ni malalamiko kutobainisha kosa la mlalamikiwa wala sehemu lilipofanyika.
“Lakini pia malalamiko haya hayajamtaja mwathirika wa tukio hilo na jina ambalo limetumika la XY halikupaswa kutumika kwa kuwa mwenye mamlaka ya kutoa idhini ya kutumika kwa jina hilo ni mahakama pekee. Mlalamikaji hakuzingatia hilo na kutumia jina hilo kinyume na utaratibu za kimahakama,” alisema Tungaraja.
Kadhalika, alisema dosari nyingine ni namna mlalamikaji alivyoandika malalamiko hayo kuwa ni baina ya mlalamikaji na mshtakiwa, jambo ambalo si sahihi.
“Alipaswa kuandika kuwa ni malalamiko baina ya mlalamikaji na mlalamikiwa, lakini yeye ameandika kuwa ni mshtakiwa wakati mtu anakuwa mshtakiwa hadi iwapo hati ya mashtaka, hivyo mahakama hii inatupilia mbali malalamiko hayo na nafasi ya kukataa rufani iko wazi,” alisema.
Septemba 5, mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma, iliahirisha shauri lililofunguliwa na Wakili Kisabo dhidi ya Afande Fatma anayetuhumiwa kuwatuma vijana kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, mkoani Dar es Salaam.
Kuahirishwa kwa shauri hilo kulitokana na hakimu aliyekuwa anasikiliza kuhamishwa kituo cha kazi, huku likiwa halijapangiwa hakimu mwingine.
Shauri hilo lilipangwa kusikilizwa Septemba 5, mwaka huu, katika mahakama hiyo na Hakimu Mkazi Fransis Kishenyi.
Kigondo alikuwa anakabiliwa na shtaka la kubaka kwa kundi kinyume na Kifungu cha Sheria Namba 131 A kifungu kidogo cha pili ambacho kinasema, anayewasaidia wahalifu kutenda kosa la ubakaji na yeye anahusika katika ubakaji wa kundi.
Hata hivyo, katika kesi namba 23476 ya mwaka 2024 ya ubakaji kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Zabibu Mpangule, ilitolewa hukumu yake, Septemba 30, mwaka huu.
Katika hukumu hiyo, washtakiwa wote walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela na kulipa Sh. milioni moja kwa kila mmoja na adhabu zote zinakwenda kwa pamoja.
Waliohukumiwa kifungo hicho ni pamoja na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Clinton Damas, maarufu kama Nyundo, askari Magereza Praygod Mushi, Nickson Jackson maarufu kama Machuche na Amin Lema, maarufu kama Kindamba.
Wote kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti huyo aliyetambulishwa kwa jina la XY.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED