WAKATI wananchi katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam wakilalamikia kukosa huduma ya majisafi takribani miezi miwili, wanaopata baadhi wanasema yamekuwa yakitoka machafu.
Maeneo ambayo yanalalamikiwa kuwa na ukosefu wa maji kwa muda huo ni Mbezi Juu, Kinyerezi, Tabata Segerea, Kiluvya, Goba na Kimara, huku yanayopata lakini hutoka machafu ni pamoja na eneo la Mwenge.
Baadhi ya wananchi wakizungumza na mwandishi wa habari hii, walikiri kupata changamoto hizo za maji katika maeneo yao.
Mkazi wa Mtaa wa Zimbili, Tabata Kinyerezi, Rhoda Alphonce, alisema wana changamoto kubwa ya maji kwa sababu kwa sasa ni takriban miezi miwili hayatoki.
Alisema licha ya kuwasilisha malalamiko yao Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) lakini mpaka sasa kero hiyo haijatatuliwa na hawafahamu sababu.
“Wale wasoma mita tuliwazuia kuja kusoma ankara za maji kwa sababu kwa miezi miwili hupati maji. Tunaishi kwa kununua maji kwenye magari,” alisema.
Victor Benard, mkazi wa Goba eneo la Mji Mpya, alisema katika maeneo yao hukosa huduma ya maji hata miezi mitatu.
Mkazi wa Mwenge, Mary James, alisema pamoja na kupata huduma ya maji, lakini yamekuwa yakitoka machafu na wakati mwingine yakiambatana na harufu na hali hiyo imekuwa ikijirudia kwa muda mrefu sasa.
“Unaletewa ankara ya maji ya Sh. 40,000 halafu ukiangalia ndani ya huo mwezi umelazimika kumwaga maji mengi kutokana na kuwa machafu na wakati mwingine hutoka yakiwa na tope unajiuliza hii ni huduma ya majisafi ama majitaka,” alisema.
Mary aliiomba mamlaka husika kuongeza umakini kwa kuhakikisha huduma wanazotoa kwa wananchi hazigeuki kuwa kero kwao hasa hizo zinazomlazimisha mtumiaji kulipia.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Magdalena Mushi, mkazi wa Tabata Barakuda, ambaye analalamika kuwa tangu utaratibu wa kutoka kwa maji kubadilika na kuwa mara moja kwa wiki, wamekuwa wakikumbana na tatizo la maji machafu kutoka bombani.
“Kuna siku yanatoka yakiwa na rangi ya udongo, siku nyingine rangi nyeusi ambayo huambatana na harufu mbaya. Inatulazimu kuyatumia baada ya kuyawekea dawa,” alisema.
Jumanne ya wiki hii (Desemba 10), DAWASA ilitaarifu kuwa wananchi wanaohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu watakosa huduma kwa saa 24 kuanzia Desemba 10 hadi 11, mwaka huu, kutokana na matengenezo ya bomba kubwa la inchi 40 linalosambaza maji katika maeneo hayo.
Ilitaja maeneo yatakayoathirika kuwa ni Chalinze, Kijini cha Mboga, Ruvu Darajani, Ruvu JKT, Vigwaza, Mlandizi, Mbwawa, Visiga, Maili 35, Misugusugu, Kongowe, Soga, Miembe Saba, Kwa Mfipa, Mwendapole, Tanita, Kwa Mathias, Kwa Mbonde, Picha ya Ndege, Lulanzi na Kibaha.
Maeneo mengine ni Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Magari Saba, Mbezi Inn, Mbezi, Kimara, Tabata, Segere, Kinyerezi, Kisukuru, Bonyokwa, Msigani, Maramba Mawili, Kimara B, Kimara Korogwe, Bucha, Baruti, Ubungo, Magomeni, Ukonga, Uwanja wa Ndege, Kiwalani, Vingunguti, Gongo la Mboto, Pugu na Kisarawe.
Mkazi wa Kiluvya, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Ally Mohamed, alisema tatizo la maji katika eneo hilo lilianza tangu Desemba 7, mwaka huu na si Desemba 10 kama mamlaka hiyo ilivyoutaarifu umma.
Alisema kwa sasa wanatumia maji ya chumvi pekee ambayo pia, gharama zake zimepanda kutoka Sh. 15,000 kwa lita 1,000 na sasa imefikia Sh.25000.
“Niliagiza maji tangu juzi asubuhi, lakini yalifika jana, kwa hiyo nikalazimika kununua maji ya dukani ya lita 18 madumu matatu kwa Sh. 21,000 ya kutumia nyumbani,” alisema Miriam Gregory, mkazi wa Kimara.
Mkazi wa Mbezi Juu, Ashura Said, alisema upatikanaji wa maji katika eneo lao umekuwa wa shida ,kwani kabla ya matengenezo hayo yamekuwa yakitoka mara moja kila baada ya siku kumi.
KAULI YA DAWASA
Alipotafutwa na mwandishi wa gazeti hili kuhusiana na upatikanaji wa maji katika eneo moja la Kibamba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa DAWASA, Everlasting Lyaro, alisema ni mzuri isipokuwa kwasasa umeathiriwa na maboresho yanayoendelea katika Mtambo wa Ruvu Juu.
Alisema marekebisho hayo yatakapokamilika hali ya upatikanaji wa maji itatengemaa kata zote tano za kihuduma ambazo ni Kiluvya, Mbezi, Kibamba, Msigani na Kwembe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED