Kamati, waliogoma kupisha mgodi kuteta

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 11:25 AM Jan 30 2025
Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa.
Picha: Mtandao
Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa.

SERIKALI imesema inatarajia kuunda kamati kukutana na watu waliogoma kupisha tathmini ya eneo la mgodi wa dhahabu wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye kikao cha kupokea taarifa ya utendaji wa migodi ya Kampuni ya Barrick ya North Mara mkoani humo na Bulyanhulu  Shinyanga, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, alisema kuwa watu 11 ambao wamegoma kupisha kufanyika tathmini hiyo kabla ya uwekezaji.

"Katika kikao chetu cha ndani, tumependekeza kuunda 'Tax Force' kwa kuchukua watu kutoka wizarani, Barrick, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kukutana na wananchi waliogoma, tunaamini baada ya kikao hicho, mambo yataenda vizuri," alisema Dk. Kiruswa.

Alisema Serikali inataka makubaliano yafikiwe ili kuruhusu uwekezaji huo wa mgodi kwa faida ya taifa na wananchi wanaoishi kuuzunguka

Mgodi huo wa Barrick North Mara unafanya tathimini mpya kwa ajili ya kuongeza eneo la mgodi huo katika Wilaya ya Tarime.

Katika hatua nyingine, Serikali imesema Barrick ipo tayari kuyatafutia ithibati madini ya Tanzania ili Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iweze kuwa na madini yatakayotambulika kama fedha.

"Serikali tunaishukuru Barrick kwa kuona umuhimu wa kusaidia kupatikana kwa ithibati ya madini yetu, hii itasaidia kuliongezea taifa fedha za kigeni na faida kubwa," alisema Kiruswa.