MFANYABIASHARA Khamis Luwongo (38) amedai mahakamani kuwa alilidanganya Jeshi la Polisi kwamba alimuua na kuchoma moto mwili wa mke wake Naomi Marijani kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata, hivyo ameomba aachwe huru akamtafute kwa kuwa yupo hai.
Pia amedai kuwa upande wa Jamhuri pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali wameshindwa kuthibitisha kwamba aliyefariki dunia ni Naomi kwa sababu hakuna majibu ya vinasaba (DNA) yaliyoonesha hivyo katika ripoti iliyoletwa na shahidi.
Luwongo alidai hayo hayo juzi mbele ya Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam huku akiongozwa na Wakili wake, Hilda Mushi wakati anatoa utetezi wake katika kesi ya mauji ya mke wake inayomkabili.
Alidai kuwa mawakili wa serikali wanataka ahukumiwe kunyongwa, akihoji "vipi nikihukumiwa kunyongwa halafu baadaye mke wangu akatokea?"
Alidai, "Mke wangu hajafa kwa sababu nilichokichoma ni mabaki ya mwili uliokuwamo katika kaburi ndani ya shamba nililonunua mkoani Morogoro pamoja na mabaki ya mzoga, ndiyo maana hata ripoti ya Mkemia haijaonesha kama mabaki hayo ni ya Naomi," alidai Luwongo.
Mshtakiwa huyo alidai kuwa askari polisi na ndugu wa marehemu walikuwa wanataka maiti, akawaza atawonesha maiti gani ili aepuke mateso hayo, akawaza awapeleke sehemu yoyote yenye makaburi, akakumbuka kwenye shamba lake lililoko Morogoro.
"Nililinunua kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha kisiasa, nililifyeka nikataka kujenga nyumba ya wafanyakazi, nikachimba mashimo matano kwa ajili ya kupanda migomba ya kisasa na shimo kwa ajili ya choo," alidai mshtakiwa Luwongo.
Alidai kuwa yale majani yaliyokuwa yamefyekwa na kijana wake, walipokwenda kuyazoa wakakuta mifupa ya mzoga wa mnyama, akamwambia kijana wake akauchukue.
"Kuna eneo lingine nililokuwa nimelinunua, kulikuwa na kaburi lakini tukakubaliana na wenye eneo hilo wakalihamishe na mimi nikaanza ujenzi ili nihamie na familia yangu, lakini ule msingi ulipoharibika, nikawaambia wale vijana wachimbe udongo kwa ajili ya kufukia," alidai.
Luwongo alidai baada ya kuchimba, wakaanza kutoa mifupa akaona hao waliohamisha lile kaburi hawakuteleleza kazi yao vizuri na kwamba hiyo mifupa ni ya marehemu waliyehamisha mwili wake.
Alidai kuwa siku hiyo alikuwa na safari ya kwenda kwenye shamba la Morogoro, hivyo aliichukua mifupa hiyo akaipeleka huko kuirundika kama uchafu, na akawaambia vijana wachome moto.
"Kwa kuwa ninajua kuwa majivu ni mbolea, nikayachukua yale majivu nikapandia migomba," alidai Luwongo.
Alidai kuwa Julai 15, 2019, alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Dar es Salaam ambako aliwakuta ndugu wa mkewe, alipelekwa kwa Mkuu wa Upelelezi Camilius Wambura wakati huo, aliwakuta maofisa wengi wakubwa wa Polisi.
Alidai kuwa Kamanda Wambura alimwuliza "maiti ya mkeo iko wapi?" Kwa sababu meseji zote hizo amejitumia mwenyewe kulidanganya Jeshi la Polisi lakini yeye akasema hajui na taarifa za mkewe amefungua jalada polisi.
"Mkuu wa Upelelezi akaniambia 'sasa sisi kama Jeshi la Polisi tutakuelekeza namna maiti ya mkeo iliko'. Baada ya hapo nilivuliwa nguo zote, nikabaki uchi, nikafungwa kamba, nikaning'inizwa kwenye mabomba kichwa chini miguu juu na mwingine akawa anampiga kwenye unyayo," alidai.
Mshtakiwa huyo alidai kuwa aliomba wamwache apumzike, akiahidi kuwaambia ukweli, hivyo walimwachia na baadye wakampeleka mahabusu. Alidai kuwa kutokana na mateso yale aliyokuwa akiyapata polisi, alikumbuka yale majivu, akaona awapeleke shambani.
"Kwahiyo, ili kujiokoa na mateso hayo, nikawaambia 'hapo ndipo alipo mke wangu'. Siku hiyo, saa 10 usiku, askari wale waliniamsha niwapeleke ndipo nikaamua kutunga stori ya uongo, lakini si kweli! Kwanza, hata huo mkaa wanasema magunia mawili si kweli.
"Mashahidi wanaozungumzia huu mkaa ni kijana wangu ambaye alisema alileta viroba viwili akaviweka kwenye gari, lakini shahidi mwingine alisema alileta kiroba kimoja cha mkaa, hakuna magunia mawili ya mkaa, ni kiroba kimoja," alidai.
Alidai kuwa baada ya mkewe kutoonekana, walitumia mkaa huo kupika hadi ukaisha na mkaa mwingine aliwasha gari akaupeleka kwa mwanamke mwingine.
Akizungumzia matone ya damu yaliyokutwa pembeni mwa kitanda, chaga na ukutani alidai inawezekana ni damu za hedhi kwa kuwa alikuwa ana tabia za kuingiza wanawake katika chumba chake na pia inaweza ikawa hata damu ya mtoto wake wa kike, anaweza akawa amejikata.
"Na ndiyo maana kwenye ripoti ya Mkemia imeonesha kwamba damu hiyo ni ya jinsia ya kike. Hata mke wangu alikuwa anaingia katika siku zake kwa sababu na yeye ni mwanamke na pia hivi sina akili kiasi miezi miwili niache kufuta matone hayo ya damu," alidai
Mshtakiwa Luwonga ambaye ni mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam, anadaiwa kuwa Mei 15, 2019, akiwa Gezaulole , wilayani Kigamboni, alimuua Naomi Marijani kisha kuchoma moto mwili wake, akitumia magunia ya mkaa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED