Aweso avalia njuga upatikanaji wa maji Dodoma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:32 AM Nov 01 2024
Waziri wa Maji Jumaa Aweso.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amefanya ziara katika maeneo ya Miganga-Mkonze na Nkuhungu kuangalia hali ya upatikanaji wa maji jijini Dodoma na kutoa maelekezo kwa watendaji kuimarisha utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji ili uchimbaji visima virefu uanze kwa uharaka.

Aweso amesema jiji hilo linakabiliwa na adha ya upatikanaji wa maji iliyosababishwa na ongezeko kubwa la watu, hivyo ni muhimu kufanyika utafiti wa kuchimba visima hivyo ili kutatua hali hiyo.

“Mh Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametupatia vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji,nataka vianze kazi hiyo hapa Jijini Dodoma ili tuendelee na uchimbaji wa visima virefu kutatua adha ya upatikanaji wa maji iliyosababishwa na ongezeko kubwa la watu Jijini Dodoma.

Wakati tunasubiri mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria na Mradi wa Bwawa la Farkwa,endeleeni kuchimba visima virefu maeneo tofauti tofauti ya Jiji ili kupunguza adha ya maji hapa Dodoma.

Hakikisheni hamuwabambikizii wananchi bili za maji ni marufuku mtumishi wa mamlaka kufanya hivyo,ili kuondokana na changamoto kubwa iliyolalamikiwa ya kubambikiziwa bili ya maji,tunajiandaa kuja na mfumo wa kulipa maji kadri utakavyotumia“ amesema Aweso

Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.
Naye, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amemshukuru Waziri Aweso kwa jitahada kubwa za utatuzi wa kero ya maji jijini Dodoma na kuomba  utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa maji wa Nzuguni A ambao utasaidia upatikanaji wa maji katika maeneo ya Ihumwa,Nzuguni,Ilazo,Mlimwa C,Kisasa,Mailimbili,Area C,Area D na Chamwino.

Awali, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA) Mhandisi Aron Joseph amesema mahitaji ya maji jijini Dodoma kwa siku ni lita Milioni 147  huku uzalishaji ni lita Milioni 79 na hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 68.
1