HATIMA ya mshtakiwa wa kesi ya kuwatuma vijana kumbaka na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya Dar es Saalam, Fatma Kigondo maarufu kama ‘Afande’ kuendelea kubaki mtaani kujulikana wiki ijayo.
Wakili wa upande wa mlalamikaji, Peter Madeleka, aliiomba Mahakama ya Wilaya Dodoma kutoa amri ya kumkamata na kumweka rumande mshtakiwa huyo kwa ajili ya usalama wake kama ilivyofanya kwa washtakiwa wengine.
Fatma, anakabiliwa na shtaka la kubaka kwa kundi kinyume na kifungu cha sheria namba 131 A, kifungu kidogo cha pili ambacho kinasema anayewasaidia wahalifu kutenda kosa la ubakaji na yeye anahusika kwenye ubakaji wa kundi.
Kesi hiyo ambayo ilipangwa kusikiliza jana, iliahirishwa hadi Oktoba 15, mwaka huu, baada ya mshtakiwa kutofika mahakamani kwa madai kuwa ni mgonjwa.
Wakili, Madeleka akiwasilisha hoja zake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Nyambuli Tungaraja, aliiomba mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa Fatma na kumweka rumande katika Gereza la Isanga jijini hapa.
Wakili, Madeleka alidai mahakamani hapo kuwa kutoa amri hiyo ili mshatakiwa huyo akamatwe mara moja na kunyimwa dhamana kama ilivyokuwa kwa washtakiwa wengine.
"Mheshimiwa hakimu tunaomba mahakama yako tukufu itoe amri ya mshtakiwa kukamatwa na kuwekwa rumande na kuondolewa dhamana kwa sababu ya usalama wake kama ambavyo mahakama imekuwa ikitoa amri hizi kwa washtakiwa wengine.
“Lakini pia kutokana na mshtakiwa leo (jana) kutofika mahakamani hapa amevunja amri ya mahakama ambayo inamtaka kufika kila tarehe ya shauri lake, hivyo tunaomba mahakama itoe adhabu kali mara moja kwa mshtakiwa kuvunja amri ya mahakama ya kumtaka kufika kila shauri linapoendeshwa kwani kukosekana kwake hapa leo kesi hii haiwezi kuendelea,” alisema Madeleka.
Wakali wa mlalamikiwa, Sedrick Mbunda, awali alieleza mahakama hiyo kuwa mteja wake hajafika mahakamani kutokana na ugonjwa na kuiomba mahakama impangie siku nyingine ya kusikilizwa shauri hilo.
Hoja hiyo ilipingwa na wakili Madeleka ambaye alihoji kama mshtakiwa huyo ni mgonjwa kwanini wakili huyo hajaleta ushahidi wa daktari mbele ya mahakama hiyo.
“Kama anaumwa lazima wangeleta ushahidi wa daktari kama ambavyo wanatakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria, lakini hii kusema tu mtu anaumwa sio kazi ya mahakama kubaini kama mtu anaumwa kweli au haumwi, walipaswa kuleta ushahidi wa kimatibabu hapa sio kuzungumza tu,” alisema Wakili Madeleka.
Hakimu Tungaraja, aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 15, hoja hizo zitakapotolewa uamuzi.
Septemba 5, mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma iliahirisha shauri lililofunguliwa na Wakili Paul Kisabo dhidi ya Afande Fatma Kigondo anayetuhumiwa kuwatuma vijana kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.
Kuahirishwa kwa shauri hilo kulitokana na hakimu aliyekuwa anasikiliza shauri hilo kuhamishwa kituo cha kazi huku shauri hilo likiwa halijapangiwa hakimu mwingine.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED