Vijana VETA washauriwa kutumia ujuzi, bunifu kutatua changamoto za kijamii

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 03:38 PM Nov 08 2024
Mkurugenzi wa Asma Mwinyi Foundation (AMF) Asma Mwinyi (wakwanza kulia) akipokea maelezo mbalimbali kutoka kwa mwanafunzi wa chuo cha VETA Pwani.
Picha Maulid Mmbaga.
Mkurugenzi wa Asma Mwinyi Foundation (AMF) Asma Mwinyi (wakwanza kulia) akipokea maelezo mbalimbali kutoka kwa mwanafunzi wa chuo cha VETA Pwani.

MKURUGENZI Mkuu wa Asma Mwinyi Foundation (AMF) Asma Mwinyi ametoa wito kwa vijana wa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) Pwani na taifa kwa ujumla wanaohiti na wale wanaoendelea na masomo kutumia vizuri fursa ya ujuzi na kufanya bunifu zitakazoenda kutatua changamoto zilizoko katika jamii.

Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kuleta maana halisi ya kaulimbiu inayesema (Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa uchumi endelevu) akieleza kwamba ujuzi na bunifu ni nyezo muhimu katika taifa lolote linalohitaji maendeleo.

Wito huo ameutoa leo Novemba 7, 2024 wakati akihutubia katika mahafali ya 14 ya Chuo cha VETA Pwani, ambako alishoriki kama mgeni rasmi. 

"Nitumie nafasi hii pia kutoa wito kwa taasisi mbalimbali kuiga mfano wa Serikali kwa kusaidia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wenye uhitaji hasa wale wanaotoka kwenye mazingira magumu," anesema Asma. 

Aidha, katika Mahafali hayo, Asma ameahidi kutoa mifuko 100 ya Saruji kwaajili ya kwenda kusaidia kuboresha miundombinu ya kijifunzia katika chuo hicho.

Naye, Makamu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Pwani Clara Kibodya ameziomba asasi zisizo za kiserikali na wadau mbalimbali kuendelea kufadhili vijana walio katika mazingira magumu kwa kutambua mahitaji yao na kisha kuwapeleka VETA ili kupatiwa mafunzo elimu ya ujasiriamali.

Amesema mafunzo hayo yatawatengenezea fursa za kujiajiri au kuajiriwa katika sekta rasmi na zisizo rasmi na kwamba hiyo itapunguza wimbi la vijana wasio na ajira. 

"Mafunzo ya VETA huendeshwa kwa mfumo wa ufundi mahiri ambao unalenga na kuzingatia ujuzi unaoendana na soko la ajira. Muundo mzima wa mafunzo humpatia mwanafunzi mazoezi mengi ya vitendo, elimu ya nadharia na tabia, sambamba na mafunzo viwandani, hivyo yatasaidia vijana wetu kutumia ujuzi watakaupata kujitengenezea kipato," amesema Clara.