UKAGUZI wa kiufundi na kiufanisi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato, jijini Dodoma uliofanywa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), umebainisha dosari kadhaa katika utekelezaji wake.
Miongoni mwa dosari hizo ni ongezeko la gharama za ujenzi kwa Sh. bilioni 6.97 kutokana na sababu mbalimbali na adhabu ya riba ya Sh. milioni 322.721 kutokana na kucheleweshwa malipo kwa makandarasi.
Kufuatia dosari hizo, Bunge limeazimia ifanyike tathmini ya kina ya hasara zilizotokana na dosari za awali za usanifu na kuweka uwajibikaji wa gharama zilizozalishwa kwa pande zinazohusika na mkataba.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, akiwasilisha bungeni jijini hapa jana taarifa ya shughuli zilizofanywa na kamati yake kwa mwaka unaoishia Februari 2025, alisema ukaguzi ulibaini kuwapo ongezeko la malipo ya Sh. bilioni 5.729 kwa mkandarasi kwa kazi ambazo hazikuidhinishwa na Bodi ya Zabuni.
"Mapitio ya hati ya malipo ya kazi za ujenzi namba tisa kwa mkataba wa kwanza kwa ajili ya kazi za miundombinu ambayo ilihusisha malipo ya hati zilizopita (hati namba moja hadi hati namba nne), yalionesha malipo ya Sh. bilioni 5.729 kutokana na mabadiliko ya kazi katika vipengele vya makadirio ya gharama za ujenzi wa mradi bila kupata idhini ya Bodi ya Zabuni," alisema.
Kaboyoka alisema dosari zingine ni kuchelewa mchakato wa kumpata mkandarasi wa pili (anayehusika na ujenzi wa miundombinu ya majengo mbalimbali), hali ambayo itasababisha ongezeko la gharama kutokana na nyongeza ya mkataba wa mshauri elekezi anayesimamia ujenzi wa uwanja huo.
Alisema Bunge linaazimia serikali ifanye mapitio ya vipengele vya mikataba ya makubaliano ya ufadhili ili kuweka usawa wa malipo ya gharama zinazoongezeka kwa kuhakikisha upande uliosababisha ongezeko hilo unawajibika.
"Bunge linaazimia serikali ihakikishe Wizara ya Ujenzi na TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania) wanasimamia kikamilifu mradi na kufanya tathmini ya kina kuhusu hasara zilizotokana na dosari za awali za usanifu, ikiwa ni pamoja na kuweka uwajibikaji wa gharama zilizozalishwa kwa pande zinazohusika na mkataba," alisema.
Alisema wanaazimia TANROADS ihakikishe kazi zilizoongezeka na zitakazoendelea kuongezeka, zinaidhinishwa na Bodi ya Zabuni kwa mujibu wa masharti ya mikataba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kudhibiti ongezeko la gharama.
"Gharama za ujenzi wa mradi huu zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 329.47, makubaliano ya muundo wa ufadhili wa mradi huo yalifanyika Machi 13, 2020 ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ilikubali kutoa mkopo kwa Serikali ya Tanzania wa Dola za Marekani milioni 271.63 na Serikali ya Tanzania ilitarajiwa kuchangia Dola za Marekani milioni 57.84," alisema.
Mwenyekiti huyo pia alisema matokeo ya ukaguzi huo wa kiufundi katika uwanja huo yamebaini kutumika kwa wahandisi ambao hapo awali hawakuwa wamesajiliwa na mamlaka husika za kitaalamu katika utekelezaji mradi.
"Ukaguzi ulibaini kuanza ujenzi wa majengo bila ya kuwa na hatimiliki na vibali vya ujenzi na kuwa jambo hilo lilikuwa kinyume cha matakwa ya Kanuni Na. 4 ya Kanuni za Ujenzi wa Mipango Miji ya Mwaka 2018," alisema.
Kanuni hiyo inaelekeza ujenzi wowote lazima upate kibali cha ujenzi kinachotolewa na mamlaka ya upangaji kulingana na michoro ya ujenzi iliyoidhinishwa na mamlaka ya mji husika.
Pamoja na hayo, Kaboyoka alisema ukaguzi ulibaini changamoto katika upembuzi yakinifu wa kina, hali iliyosababisha ongezeko la gharama Sh. bilioni 3.04.
Alisema kwa mujibu wa sehemu ya 3.3 ya Mwongozo wa Usanifu wa Kijiometri wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi wa Mwaka 2011, upembuzi yakinifu unapaswa kufanyika kwenye masuala ya hali ya udongo, kiwango cha mteremko kwenye eneo la mradi, gharama za ujenzi na uchaguzi wa njia ya kupitisha barabara.
Alieleza tofauti katika vipimo hivyo ilitokana na mbinu iliyotumika wakati wa upembuzi yakinifu ambapo ndege nyuki (drones) zilitumika kupima mwinuko wa usawa wa ardhi bila kusafisha eneo la mradi, hivyo kutotafsiri kwa usahihi kuwa usawa wa vichaka kama ndiyo usawa wa ardhi.
Alisema hali hiyo ilisababisha kuathiriwa kwa utekelezaji mradi kutokana na tofauti kati ya viwango halisi vya mwinuko na viwango vya michoro.
Kuhusu kuchelewa kwa malipo ya mkandarasi, alisema malipo ya mradi yalicheleweshwa kwa muda wa kati ya siku nane hadi siku 70, hata kusababisha gharama zilizotokana na riba kuongezeka.
Alisema Serikali ya Tanzania ilitakiwa kulipa riba hizo kulingana na makubaliano yake na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na ukaguzi ulibaini katika mchakato wa ununuzi, TANROADS iliidhinisha ombi la mapendekezo ya mradi (RFPs)5 ambayo hayakukamilika.
Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Stephen Byabato, akichangia hoja hiyo ya kamati, alisema "Uwanja wa Msalato kuna ucheleweshaji wa mradi unaoongeza fedha zinazodaiwa tutakuja kupata shida kuzilipa na kwa misingi hiyo pale mjini Bukoba, nimejengewa control tower, haijaanza kwa mazingira haya ya kuchelewesha."
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Anatropia Theonest, alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya kukosewa kwa usanifu wa miradi ya serikali, jambo ambalo limeongeza gharama kutokana na riba.
Alisema katika uwanja huo gharama za ujenzi ziliongezeka zaidi ya Sh. bilioni tano ambazo zingeweza kutumika kugharamia miradi mingine ya umma.
Akichangia taarifa hiyo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga aliwahakikishia wabunge wizara zote za kisekta zitakwenda kuyafanyia kazi ushauri na maazimio ya Bunge.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED