MMILIKI wa Kituo cha Cambiasso Sports Academy, Kambi Zuberi Seif na aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba, Muharami Sultan, wameieleza mahakama kuwa walikiri kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kutokana na mateso waliyopewa, ikiwamo kuvuliwa nguo zote na kuning'inizwa juu.
Aidha, wamedai kuwa hata walipofikishwa mbele ya mlinzi wa amani katika Mahakama za Mwanzo, walilazimishwa kutia saini maelezo ambayo hawakuyatoa, na kutishiwa kuwa wasipotia saini wangeuawa.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin ambao nao waliteswa kukiri mashtaka hayo ni Maulid Mzungu, maarufu kama Mbonde, Said Matwiko, Fundi Selemara na John Andrew, maarufu kama Chipanda mfanyakazi wa Cambiasso.
Pia mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo, Sara Joseph ambae ni mke wa Said, alidai kuwa tangu akamatwe mwaka 2022, hakuwahi kutia Saini nyaraka yoyote.
Washtakiwa hao walidai hayo juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada ya kumaliza kusomewa maelezo ya mashihidi Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, akisaidiana na Roida Mwakamele.
Hakimu Lyamuya aliwauliza washtakiwa kama wanachochote cha kuzungumza kama kanuni inavyotaka ndipo wakili wa mshtakiwa Kambi, Dominicus Nkwera, alipodai kuwa shahidi namba mbili na tatu ni mtu mmoja ambaye ni Innocent Masangula.
"Tunaomba iingie kwenye rekodi kwamba huyu shahidi ni mtu mmoja lakini ana maelezo mawili tofauti na tarehe tofauti," alidai Wakili Nkwera
Pia alidai kuwa iingie kwenye rekodi kwamba mteja wake, Kambi, baada ya kukamatwa aliteswa sana na maofisa polisi wa DCEA na kudhalilishwa utu wake ili akubali kutia saini nyaraka.
"Kulingana na mateso aliona bora atie saini nyaraka za kukiri kosa kuokoa maisha yake na hata alipopelekwa kwa mlinzi wa amani, walimtishia kwamba asipotia saini maelezo atakayoyakuta huko akirudi tena polisi mateso yataendelea kawa kawaida," alidai.
Mshtakiwa wa pili, Sultan, alidai kuwa alipigwa sana na kudhalilishwa mbele ya wanawake, akilazimishws kutia saini vitu ambavyo hakuvielewa na hata mlinzi wa amani aliona makovu aliyokuwa nayo mwilini.
"Nimakuuliza mlinzi wa amani kwamba narudi kule kule nilikotoka akasema ndiyo, sheria ndiyo inaelekeza hiyo, nikamwambia nikirudi wataniua," alidai Sultan.
Pia mshtakiwa Chipanda alidai kuwa alipigwa sana na akalazimishwa kutia saini maelezo.
Mshtakiwa wa nne, Said, alidai kuwa akiwa Kituo cha Polisi alilazimishwa kutia saini karatasi ambazo hazijui na Novemba 21, 2024 alisainishwa karatasi zingine Kisutu, hayo yote zilikuwa na ahadi za maofisa wa DCEA kuwa ni akikiri watamwachia mke wake, Sara.
Mshtakiwa wa tano, Maulid, aliieleza mahakama akiwa kituoni alisainishwa maelezo ambayo hayajui na pia walitweza utu wake, wakamvua nguo na wakamning'niza kwenye bomba, wakamweleza kwamba hawaoni hasara taifa likipoteza mtu mmoja.
Alidai kuwa kwa mlinzi wa amani hakuzungumza wanayoyataka wao.
Mshtakiwa Sara alidai walimchukua mume wake nyumbani wakaondoka naye baadaye walimfuata yeye wakamchukua na tangu kipindi hicho hajawahi kutia saini karatasi yoyote.
Washtakiwa walidai kuwa katika utetezi wao watakuwa na mashahidi na baadhi yao walidai watakuwa na vielelezo. Kesi hiyo itatajwa Februari 10,2025 Mahakama Kuu.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 wakiwa Kivule, Ilala mkoani Dar es Salaam, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 27.10.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kwamba Novemba 4, 2022, eneo la Kamegele, Mkuranga mkoani Pwani, kwa pamoja walikutwa wakisafirisha kilogramu 7.79 za dawa za kulevya aina ya heroin.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED