KLABU ya Singida Black Stars, amemtabiria makubwa winga wake mpya, Serge Pokou, aliyesajiliwa kutoka Al Hilal Omdurman ya Sudan, huku ikikiri kumpokea kipa, Amas Obasogie raia wa Nigeria kutoka Yanga kwa makubaliano maalum.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Hussein Masanza, amesema kuwa usajili wa Pokou, umeonekana kuwashtua mashabiki wengi wa soka nchini kwani alikuwa akitakiwa na klabu kubwa za Simba na Yanga, lakini wao wamefanikiwa kumtwaa, akisema ni mchezaji atakayetikisa ligi ya Tanzania.
"Tunajua kuwa ni mchezaji mzuri ambaye klabu kubwa za Simba, Yanga zilikuwa zinamtaka, si mgeni machoni mwa mashabiki wa soka, kwani ameshawahi kuzifunga timu hizo, kwa maana hiyo tunajua anayajua mazingira yote ya hapa nchini, angalia tulivyomtambulisha nchi yote ilitetemeka, ni usajili wa 'sapraizi' kwa wengi.
"Tunaamini si mchezaji wa kusubiri muda, kama alipokuwa akitua tu na Al Hilal anafanya balaa, basi balaa kubwa zaidi linakuja," alisema Masanza.
Pokou, raia wa Ivory Coast, alifunga bao katika mchezo wa kirafiki mwaka jana Simba ikicheza dhidi ya Al Hilal katika mchezo wa kirafiki uliochezwa, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, zikitoka sare ya bao 1-1, pia aliwahi kuifunga Yanga kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa misimu miwili iliyopita.
Mbali na mchezaji huyo, Masanza amesema wameingia makubaliano maalum na Yanga, kumchukua kipa wao, Obasogie, raia wa Nigeria.
"Kipa huyo amesajiliwa na Yanga, lakini tumemchukua kwa makubaliano maalum, haya ni masuala ya kawaida kwenye mpira wa miguu hivyo si ajabu sana," alisema.
Awali, kipa huyo alikuwa akiichezea Fasil Kenema FC ya Ethiopia, ambapo pia mara kwa mara amekuwa akiitwa kuunda kikosi cha Timu ya Taifa ya Nigeria.
Ofisa Habari huyo, ametangaza kuwasajili straika raia wa Ghana, Jonathn Sowar na Eliuter Mpepo, huku ikiachana na Joseph Guede ambaye amemaliza mkataba wake na klabu hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED