SERIKALI imeanzisha mkakati maalumu wa kukuza zao la kawaha nchini, ili pamoja na mambo mengine, liingizie nchi fedha za kigeni na kukuza uchumi wa wakulima.
Akizungumza Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Frank Nyarusi, amebainisha miongoni mwa mikakati hiyo ni kutoa ruzuku ya pembejeo kama mbolea na miche kwa wakulima.
Ameongeza kuwa, mikakati hiyo imezaa matunda na kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji wa pili wa kahawa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na ya nne barani Afrika.
“Ndani ya miaka minne uzalishaji umeongezeka kutoka tani 58,000 na kutarajiwa kufika tani 75,000 mwaka huu. Mapato nayo yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 112; na mwaka huu tunategemea kufika Dola za Marekani milioni 300,” alisema.
Amesema kahawa inauzwa kwenye minada na wakulima wanalipwa ndani ya saa 48 hadi 72.
Amesisitiza mikakati ya serikali ni inakusudia kugawa miche milioni 20 ya kahawa kwa wakulima kila mwaka, ili kuongeza uzalishaji.
Nyarusi amesema mbali ya ruzuku, mafanikio hayo yamechangiwa na kuanzishwa kwa mifumo mipya ya uuzaji wa zao hilo kupitia mnada wa mtandaoni, ambayo imeleta ushindani wa bei na kuongeza uzalishaji.
“Kuna mifumo mipya ya uuzaji wa kahawa ambayo imeleta ushindani mkubwa, kwa mfano miaka minne iliyopita wakulima walikuwa wanapata Sh. 1,500 hadi Sh. 3,000 kwa kilo moja ya kahawa aina ya robusta, lakini kupitia mnada wanapata Sh. 5,000 hadi 6,500 kwa kilo moja,” alisema Nyarusi.
Kuhusu Mkutano wa Kahawa barani Afrika (G25), uliopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam, Nyarusi amesema unatoa fursa kwa wakulima na viwanda vilivyopo kwenye mnyororo wa kuongeza thamani zao hilo, kujitangaza kimataifa kwa kuwa wadau muhimu kutoka nchi mbalimbali watashiriki.
Amesema nchini, kila ukanda unaozalisha kahawa, unatoa yenye ladha ya kipekee na kwamba wageni watapata fursa ya kuona kahawa inayozalishwa nchini.
Ametaja kanda zinazozalisha kahawa kwamba ni Kaskazini, Mara, Kagera na Kusini inayojumuisha mikoa ya Ruvuma na Songwe.
Baadhi ya wakulima akiwamo Amir Hamza, amesema wazalishaji wengi wa zao hilo Afrika husafirisha bidhaa ghafi za kahawa kwenda ulaya ambako kuna walaji wengi, kinachosababisha kupunguza thamani ya zao hilo.
Kwa mujibu wa Nyarusi, mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu ya ‘Jinsi Sekta ya Kahawa itasaidia Ajira kwa Vijana, Kuongeza Uzalishaji na Thamani ya Zao la Kahawa.’
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED