WAKONGWE wa soka la Tanzania, Simba na Yanga, leo watakuwa kwenye majiji tofauti kucheza michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakati Simba watakuwa Makao Makuu ya nchi, kucheza na wenyeji Dodoma Jiji, kwenye Uwanja wa Jamhuri, saa 12:30 jioni, Mabingwa Watetezi, Yanga wao watakuwa jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya KMC, pambano linalotarajiwa kuanza saa 3:00 usiku, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Utakuwa ni mchezo wa nne kwa Simba katika Ligi Kuu na wa tatu kwa Yanga kwa kuwa zilikuwa kwenye shughuli pevu ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na sasa zimerejea.
Simba itaingia uwanjani hapo ikiwa na kumbukumbu katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita, uliopigwa Mei 17 mwaka huu, ikipata ushindi wa bao 1-0 lililowekwa wavuni na Freddy Michael ambaye aliachwa mwishoni mwa msimu huo.
Yanga ina kumbukumbu nzuri ya kutoa kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya KMC kwenye uwanja huo huo, Agosti 23 mwaka jana, ikiwa ni mchezo mzunguko wa kwanza wa ligi ya msimu uliopita. Kocha wa Simba, Fadlu Davis, amesema itakuwa ni mechi ngumu kama zingine zote, huku akisikitika kuwakosa nyota wake ambao ni Joshua Mutale, Yusuph Kagoma na Mzamiru Yassin.
Hata hivyo, Mzamiru hajaonekana katika michezo mbalimbali ya hivi karibuni. "Itakuwa mechi ngumu kama nyingine tu zilivyokuwa, nimejaribu kufuatilia, lakini hakuna mfumo halisi ambao tutakwenda kucheza na wala walionao wapinzani wetu, tunakwenda kucheza kujaribu kupata pointi tatu.
Ninachotaka kusema ni kuwataka tu mashabiki wa Simba waliopo Dodoma waje kutusapoti, waje kuwashangilia wachezaji wao na kutusaidia kupata ushindi," alisema Fadlu, raia wa Afrika Kusini. Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Macky Maxime, amesema wamejipanga kucheza dhidi ya Simba, huku wakijua wanacheza na timu kubwa.
"Tunacheza na Simba, lakini nimeandaa vijana wangu nadhani tutawakabili vizuri na mchezo utakuwa mzuri pia," alisema. Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Moses Mpunga, amewataka mashabiki wa Simba kutokwenda na matokeo uwanjani. "Moja kati ya viwanja vigumu kwa Simba ni hiki cha Jamhuri Dodoma, huwa wanashinda lakini kwa tabu sana, wanashinda bao moja moja katika mazingira magumu, lakini nadhani safari hii hawachomoki," alisema.
Katika mchezo utakaopigwa Chamazi usiku, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema wamejiandaa vyema na mchezo huo, lakini akienda kwa tahadhari kwani anakwenda kucheza na mpinzani bora.
"Tunakwenda kucheza mchezo dhidi ya mpinzani mgumu, huwa nasema siku zote michezo hii siyo rahisi, inabidi tuwaheshimu pia wapinzani wetu. Nimeifuatiliwa msimu huu, KMC ni timu ngumu, na Ligi Kuu Tanzania kila msimu unakuwa mgumu kuliko uliopita," alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Kocha huyo amesema ingawa yeye na baadhi ya mashabiki wangependa washinde mabao mengi, lakini haitokuwa rahisi kutokana na wapinzani walivyojipanga, lakini pia wachezaji wake wanavyopoteza nafasi. "Yanga tunaingia zaidi ya mara 20 kwenye eneo la hatari la mpinzani wetu, lakini tumekuwa tukikosa sana," alisema kocha huyo.
Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin, amesema ni ngumu sana kucheza na timu kama Yanga, hivyo amewataka wachezaji wake kuwa makini na kutofanya makosa mara kwa mara.
"Unabidi tucheze mchezo huu kwa umakini mkubwa, nafikiri vijana wako tayari, nafikiri Yanga imebadilika siyo kama ile ya msimu uliopita," alisema kocha huyo raia wa Somalia. Aliwataka wachezaji wake wasifanye makosa kama waliyofanya dhidi ya Azam FC, Septemba 19 na kujikuta wakibugizwa nyumbani, mabao 4-0.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED