Rais Samia kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura Oktoba 11

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 04:23 PM Oct 06 2024
news
Picha:Shaban Njia
Waziri wa Ardhi na Mbunge Chamwino, Deogratius Ndejembi.

RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura katika Jimbo la Chamwino jijini Dodoma Oktoba 11,2024 ili kupata nafasi ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27 mwaka huu na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha nchi nzima.

Waziri wa Ardhi na Mbunge Chamwino, Deogratius Ndejembi ameyabainisha haya leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Msalala na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi hasa katika Sekta ya Ardhi.

Amesema, Rais Samia atajiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura Oktoba 11 mwaka huu jimboni kwake Dodoma ili kuweza kupata nafasi ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo atalazimika kukatisha ziara ili nae akashiriki na kuahidi kuhakikisha anatembelea miradi yote na kufikia Oktoba 30 mwaka huu.

Ndejembi amesema,kila waziri amepewa mkoa ambao atazunguka na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi ikiwemo kukagua miradi ya maendeleo hata kama haiko kwenye Wizara yake na yeye kapangiwa mkoa wa Shinyanga na kuahidi kukagua na kusikiliza kero za wananchi halamashuri zote sita za mkoa huu.