MASHINDANO ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa yameanza kutimua vumbi Machi 8, mwaka huu katika viwanja vya Tamco vilivyopo Mjini Kibaha kwa kuzikutanisha timu ya Kiduli FC na Black Six ya Jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Black Six wameibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa katika dakika 41 ya kipindi cha kwanza kupitia mchezaji wao Kelvin Madalisto aliyefunga kupitia mpira wa kichwa uliopigwa kutoka kulia mwa dimba hilo.
Kocha wa Kiduli FC Hery Kisanga , alisema kuwa mchezo wao wa kwanza wamefungwa kutokana na makosa yaliyofanywa na wachezaji wake lakini kufungwa kwao hakuwafanyi kukata tamaa .
Kisanga, alisema kuwa kwasasa wanajipanga na michezo mingine inayofuata na watakwenda kuyafanyiakazi mapungufu yaliyojitokeza na ana imani michezo ijayo itakwenda kuzaa matunda.
"Leo tumefungua mashindano haya lakini tumekubali kupoteza mchezo huu lakini tunaenda kuyafanyiakazi mapungufu yaliyojitokeza na tunaimani tutafanya vizuri,"alisema Kisanga
Kisanga ,aliwaomba washabiki wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi katika kuisapoti timu yao pale inapocheza ili hiweze kupata nguvu ya ushindi wa michezo mingine ijayo.
Kwa upande wake Kocha wa Black Six Omary Mbweze ,alisema siri ya ushindi wao ni wachezaji wake kujituma na kutumia vizuri nafasi waliyopata huku akiongoza kuwa ushindi huo umewapa nguvu ya kupambana na michezo mingine ijayo.
Hatahivyo,kituo cha Mkoa wa Pwani kimejumuisha timu zote zilizopangwa kundi B ikiwemo Singida Cluster,Black Six,Moro Kids,Stand FC,Red Angels,Gunners FC,na wenyeji Kiduli FC.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED