BAADA ya kumaliza dakika 90 za nyumbani za mechi ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini, Yanga imeweka rekodi nne kwenye Ligi Kuu Bara ambayo ilisimama kupisha kalenda ya michezo ya kimataifa.
Ikiwa inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kujikusanyia pointi 52, Yanga ndiyo timu inayoongoza kwa kushinda mechi nyingi zaidi, ikitoa sare chache, timu yenye mabao mengi, lakini pia imeshinda mechi zote ilizocheza kwenye uwanja wa nyumbani.
Kwa mujibu wa takwimu za dawati la michezo la Nipashe, Yanga imeshinda michezo 17 ambapo hakuna timu yoyote mpaka sasa iliyoshinda idadi hiyo ya michezo.
Timu hiyo imeshinda idadi hiyo ya michezo ikiwa imecheza mechi 20 tu, hivyo ni mechi tatu tu ambazo haikupata ushindi.
Mechi hizo ni zile mbili ilizopoteza dhidi ya Ihefu FC, ikifungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbarali, Oktoba 4, mwaka jana, mechi ya mzunguko wa kwanza na nyingine ni Machi 17, mwaka huu ilipofungwa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Yanga imepata suluhu mechi moja dhidi ya Kagera Sugar, Februari 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba, Kagera.
Simba na Azam zinafuatia kwa kushinda mechi nyingi kila timu ikiwa imeshinda michezo 14 mpaka sasa.
Yanga mpaka sasa inaongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi hiyo, ikiwa na magoli 49, lakini ikifuatiwa kwa karibu na Azam FC, ambayo yenye mabao 47 mpaka sasa.
Hata hivyo, Yanga ina mchezo mmoja pungufu ukilinganisha na Azam ambayo imeshacheza michezo 21.
Yanga imetoa sare moja tu mpaka sasa, Simba ikiwa na sare tatu na Azam tano.
Takwimu pia zinaonyesha Yanga imeshinda michezo yote 12 iliyocheza nyumbani, huku nane ikicheza ugenini ikifanya idadi ya mechi zake kuwa 20.
Katika mechi nane ilizocheza ugenini, imeshinda mechi tano, imepoteza mbili na sare moja.
Hata hivyo, timu hiyo imepoteza mechi mbili sawa na Simba na Azam ambazo zote zimepoteza idadi sawa za mechi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED