ZIKIWA zimebaki siku tano kabla ya mchezo wao wa kwanza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wachezaji wa Yanga wameanza mazoezi maalum ya 'Gym' kwa ajili ya kuongeza nguvu ya miili yao.
Wachezaji hao wa Yanga wamepangiwa muda maalum wa kufanya mazoezi hayo chini ya kocha wao wa viungo Mmorocco Taibi Lagrounihuku pia wakiendelea na mazoezi ya uwanjani.
Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi akizungumza na Nipashe, amesema mazoezi hayo ni moja ya programu maalum kuelekea kwenye mchezo huo muhimu.
"Kuna vitu nataka kuviongeza kwa wachezaji, mchezo unaofuata ni mchezo muhimu sana, ni lazima kujipanga vizuri na kuhakikisha tunakuwa kamili kwa asilimia zote, mazoezi ya gym yatawaongezea nguvu wachezaji lakini pia tunafanya mazoezi ya kutafuta kasi," amesema Gamondi.
Amesema wanaendelea na mazoezi yao bila kusikiliza maneno ya watu au kuangalia nini mpinzani wao anafanya.
"Maandalizi yanaendelea, kwa sasa hakuna muda wa maneno, ni kujiandaa tu na mechi, kimbinu na kiufundi, nataka wachezaji wangu waelekeze akili zao kwenye mchezo wetu ujao," amesema kocha huyo.
Aidha, amesema yeye (Gamondi) na wenzake kwenye benchi la ufundi tayari wameandaa mbinu za kuimaliza Mamelodi Sundowns kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
"Tuna michezo miwili dhidi yao, kila mchezo utakuwa na mbinu zake, akili yetu kwanza ipo kwenye mchezo huu wa nyumbani baada ya hapo tutajipanga kwa mchezo wa marudiano ugenini," amesema Gamondi.
Wakati huo huo, Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison amesema wapo kwenye maandalizi makali kwa sababu ni mechi ambayo itakwenda kuamua hatma ya klabu yao kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.
Walter amewata wanachama na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mechi hiyo.
"Hili jambo tusiwaachie wachezaji tu peke yao, mashabiki nao wanatakiwa wawe sehemu ya historia ya mechi hii kubwa, tunawahimiza waje kwa wingi uwanjani kuwapa nguvu wachezaji," amesema Walter.
Yanga inatafuta kuweka rekodi mpya ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukaa miaka 25 bila kufika hata hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya vilabu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED