BAADA ya kuchapwa mabao 3-1 na Maafande wa Mafunzo FC katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar iliyochezwa kwenye Uwanja wa nje wa Amaan (Annex B), Kocha Msaidizi wa Tekeleza, Juma Salum, amesema washambuliaji ndio tatizo katika kikosi chake.
Tekeleza kutoka Pemba imepoteza mechi ya pili mfululizo kwenye uwanja huo na kuendelea kujiweka katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Salum, alisema timu yake bado inakabiliwa changamoto ya wachezaji wa eneo la mbele kutokuwa na uzoefu na hivyo wanapoteza umakini.
Kocha huyo alisema licha ya kufanikiwa kumiliki mpira kwa muda mrefu, lakini wanashindwa kutumia vyema nafasi wanazopata.
Aliongeza wataendelea kuwapa mbinu mpya, ili kuhakikisha hawapotezi pointi katika mechi nyingine tisa zilizobaki za mzunguko huu wa kwanza.
“Tunafanikiwa kuwanyang’anya mipira wapinzani wetu, tunatamba nao kwa muda mrefu, lakini wachezaji wanashindwa kupeleka mbele na kufunga, sijajua ni uoga au kupoteza umakini, najua timu yangu ni changa katika Ligi Kuu Zanzibar, tunawaomba mashabiki wawape muda wachezaji, ili kuzoea mikikimikiki ya ligi hii," aliongeza kocha huyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED