WAKATI michuano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati chini ya miaka 20 ikitarajiwa kufanyika Tanzania Oktoba 6 mwaka huu, Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Charles Mkwasa, amesema kwa maandalizi aliyoyafanya anaimani watafanya vyema, ikiwemo kuubakisha ubingwa huo hapa nchini.
Akizungumza wakayi wa mazoezi ya timu hiyo, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, Mkwasa, amesema anafurahi kuona vijana wake wanapambana sana kwenye mazoezi, hivyo kumpa uwanda mpana wa kuchagua kikosi bora cha mwisho kabla ya michuano kuanza.
"Vijana wanapambana sana, wapo vizuri, tunaendelea na mazoezi kwa ajili ya kuchuja kikosi, tuko asilimia kama 70 hivi tunaangalia, ila kwa sasa tutahitaji mchezo mmoja wa kirafiki, kabla ya kuanza mashindano, nimeridhika na maendeleo ya kikosi changu, nadhani mpaka michuano ianze tutakuwa fiti na tutafanya vyema kwenye mashindano haya, hata kutwaa ubingwa," alisema Mkwasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri huo, itacheza Oktoba 6 dhidi ya Kenya kwenye Uwanja wa KMC Complex, ambapo kabla ya hapo, kutakuwa na mchezo kati ya Sudan dhidi ya Djibouti.
Taarifa hiyo imesema kuwa michuano hiyo itachezwa kwenye makundi mawili, ambapo Kundi A litakuwa na timu za Djibouti, Kenya, Rwanda, Sudan na Tanzania, huku Kundi B litauiwa na timu za Burundi, Ethiopia, Sudan Kusini na Uganda.
Timu mbili za kwanza kwenye kila kundi zitacheza nusu fainali, Oktoba 18, kabla ya fainali kupigwa Oktoba 20.
Mara ya mwisho michuano hiyo ilichezwa 2022 nchini Sudan, ambapo Uganda ilitwaa ubingwa kwa kuichapa Sudan Kusini mabao 2-1, mechi iliyopigwa Novemba 11, Uwanja wa Al Hilal nchini humo, Tanzania ikiishia hatua za makundi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED