Gamondi aiendea chimbo Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 12:19 PM Oct 06 2024

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha:Mtandao
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema muda wa wiki mbili uliosalia unatosha kabisa kuwasoma na kuwaangalia wapinzani wake Simba, kabla ya kupanga mikakati kwa wachezaji wake kukabiliana nao, Oktoba 19, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Gamondi, alisema pamoja na kwamba hufanya maandalizi katika kila mchezo, lakini unaofuata ni wa dabi na anataka kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo ambayo siku zote wako nyuma yao kuwasapoti.

"Nadhani sasa wanachama na mashabiki wa Yanga wamerejesha furaha yao baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Pamba, sasa tunakwenda kucheza na Simba, ni muda mrefu bado, ni kama wiki mbili mbele, tutajiandaa kikamilifu, sisi tunajiandaa kwa michezo yote, lakini hii ni dabi, ni muda sasa wa kukaa na kuwasoma taratibu na kuwawekea mikakati ya kukabiliana nao, huu utakuwa mchezo mzuri na zawadi kwa ajili ya mashabiki wetu ambao wamekuwa bega kwa bega na sisi kutusapoti kila tunapokwenda," alisema kocha huyo raia wa Argentina.

Alikiri kuwa hautokuwa mchezo rahisi kwani siku zote dabi haijawahi kuwa rahisi, lakini akifurahi zaidi kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao unaruhusu aina yoyote ya mfumo ambao kocha anauhitaji.

"Nadhani tutacheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, utakuwa mchezo mzuri, utakuwa mgumu, lakini tuna furaha kucheza mchezo huo, kila timu itacheza vizuri kutokana na aina ya uwanja, kwa maana hiyo kwetu sisi tutajiandaa vuzuri zaidi ili kupata ushindi," alisema. Mchezo huo utachezwa miezi miwili tu baada ya mchezo uliopita kati ya watani hao wa jadi uliopigwa, Agosti 8, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ikishinda bao 1-0, lililofungwa na Mkongomani Maxi Nzengeli, katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, wiki moja kabla ya kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Utakuwa pia ni mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo Yanga itataka kuendeleza ubabe wake, baada ya kushinda mechi zote mbili za ligi msimu uliopita.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Yanga iliichakaza Simba mabao 5-1, mechi ikipigwa Novemba 5, 2023, na mzunguko wa pili, ikashinda tena mabao 2-1, mechi ikichezwa Aprili 20 mwaka huu.

Kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikishinda michezo yote minne iliyocheza, ikikusanya pointi 12, mabao manane na haijaruhusu wavu wake kuguswa.