Fadlu apagawa viwango wachezaji wake

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 08:56 AM Oct 27 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

BAADA ya juzi kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Namungo FC, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameonekana kufurahishwa na viwango vya wachezaji wake, licha ya kwamba alifanya mabadiliko ya kikosi kwa kiasi kikubwa.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini, alisema alitarajia kuwa wachezaji wake watacheza soka safi, lakini si kwa kiasi ambacho amekiona katika mchezo huo, huku akipagawa na uwezo wa baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa hawaanzi mara kwa mara.

Katika mchezo wa juzi, kocha huyo aliwaanzisha wachezaji ambao huwa hawapati sana nafasi ya kucheza kama Chamou Karaboue, Velentine Nouma, Fabrice Ngoma, Agustine Okejepha, Steven Mukwala, Awesu Awesu na Ladack Chasambi ambao waliwashangaza mashabiki wa Simba waliojazana kwenye uwanja huo kwa kuonesha kiwango cha hali ya juu.

"Ulikuwa ushindi muhimu baada ya ule wa Mbeya dhidi ya Prisons, tumepumzika siku mbili tu kabla ya mchezo huu.

Ulikuwa ni wakati mzuri wa kumuona Valentino Nouma akirejea dimbani baada ya muda mrefu, nimefanya mabadiliko kwenye kikosi, ili kuwapumzisha baadhi ya wachezaji kwani wamecheza michezo mingi, wamenishangaza kwa kweli, Ngoma alikuwa kiongozi mzuri uwanjani, Okejepha angeweza kuwa mchezaji bora wa mechi, Mukwala ameonesha kiwango cha juu na kusababisha mabao mawili, Awesu, alikuwa kwenye kiwango bora bahati mbaya akaumia, Chasambi alikuwa hatari mno pale mbele kwa wapinzani," alisema kocha huyo.

Fadlu pia alionekana kufurahishwa na kiwango cha Joshua Mutale ambacho alisema kilikuwa cha hali ya juu na kuwapa tumbo joto wapinzani kila alipokuwa akigusa mpira na kuamua kumchezea madhambi mara kwa mara.

"Hii inanipa wakati mzuri wa mimi kama kocha kuwa na machaguo mapana, kila mchezaji sasa anatakiwa kuonyesha kiwango chake, kila mchezaji anatakiwa kutoa mchango kwenye kikosi hiki, kwa ajili ya kupata mafanikio," alisema.

Wakati Fadlu akipagawa na viwango vya wachezaji wake, Kocha msaidizi wa Namungo, Ngawina Ngawina, ambaye aliendelea kukaa benchini kama Kocha Mkuu, huku Juma Mgunda aliyetangazwa juzi akiwa jukwaani, alikiri kuzidiwa mbinu na wapinzani wake, huku akiwapongeza kwa ushindi huo.

"Tumepoteza mchezo tuwapongeze wapinzani wetu, wamepata pointi tatu ambazo wanastahili, tumefungwa kwa sababu mipango yetu haikufanya kazi, tulivyokuja kucheza tulijua ubora wao tulijaribu kukaa nyuma kwanza, lakini tukaruhusu bao la mapema kila kitu kikaharibika ilibidi tutoke nyuma, mfumo wote ukaharibika," alisema Ngawina.

Simba iliyofikisha pointi 19 kwa michezo saba iliyocheza itashuka tena dimbani, Jumanne kucheza dhidi ya JKT Tanzania kwenye uwanja huo huo, huku Namungo yenye pointi sita ikiwa kwenye nafasi ya 13 inatarajia kucheza mechi yake ya kesho dhidi ya Pamba Jiji, kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi.