USHINDI ni kauli ya makocha wa pande zote kuelekea kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo kati ya Azam FC dhidi ya Coastal Union, utakaochezwa majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Azam Complex.
Azam itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuichapa timu ya KMC mabao 4-0 katika mchezo wao uliopita ambao ulichezwa Septemba 19 mwaka huu kwenye uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Akizungumzia mchezo huo jana, Kocha Mkuu wa timu ya Azam, Rachid Taoussi alisema wamejipanga vema kuhakikisha wanapata pointi tatu katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.
"Kila mchezaji ana morali ya juu kuelekea kwenye mchezo huo kwa maelekezo na mbinu nilizowapa wachezaji wangu naamini tutapata pointi tatu katika uwanja wetu wa nyumbani,”alisema Taoussi.
Kwa upande wake Lusajo Mwaikenda ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake alisema wamejipanga vema kuhakikisha wanaendeleza ushindani waliouonesha walipokutana na KMC.
Alisema licha ya kuwa Coastal Union ina wachezaji wazuri watafuata maelekezo waliyopewa na benchi lao la ufundi ili wapate matokeo mazuri.
Kwa upande wake Kaimu Kocha Mkuu wa Coastal Union, Joseph Lazaro alisema amewaandaa vizuri wachezaji wake ili wapate ushindi japo anafahamu wanakutana na timu nzuri.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED