Waajiri Health Bonanza yatia fora, Waziri Kikwete atoa ujumbe mzito

By Frank Monyo , Nipashe Jumapili
Published at 02:15 PM Oct 20 2024
Waajiri Health Bonanza yatia fora, Waziri Kikwete akumbusha kupima afya mara kwa mara
Picha: Mpigapicha Wetu
Waajiri Health Bonanza yatia fora, Waziri Kikwete akumbusha kupima afya mara kwa mara

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Jakaya Kikwete ametoa wito kwa waajiri na Wafanyakazi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kupunguza athari zinazotokana na magonjwa ya kuambukiza kama kisukari na shinikizo la damu.

Kauli hiyo ameitoa jana Oktoba 19,2024 wakati wa Tamasha la Waajiri Health Bonanza lilioandaliwa na ATE  lililofanyika katika viwanja vya mchezo vya Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.

Kauli mbiu ya bonaza hilo lilikuwa ni “Zuia magonjwa yasiyoambukiza, ongeza ufanisi kazini”. 

Waziri Kikwete alisema kuwa mapambano ya magonjwa yasiyoambikizwa yanahitaji nguvu ya pamoja ili kuyatokomeza.

"Kwa kuzingatia hilo serikali kwa kushirikiana na wadau inafanya kampeni na maadhimisho ya kitaifa kwaajili ya kuhamasisha jamii kuhusu kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara" alisema na kuongeza kuwa;

"Takwimu zinaonesha wenye umri kuanzia miaka 30 na kuendelea wanashinikizo la juu la damu, kisukari na uzito uliozidi ingawa serikali ndio inategemea nguvu kazi hiyo." alisema 

Alisisitiza waajiri wote kuzingatia sheria ya usalama wa afya mahala pa kazi na kujenga mazingira wezeshi kwa watu wote hususani watu wenye ulemavu ili kuwa na uchumi shirikishi na wa ushindani.

Waziri Kikwete aliwapongeza Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kuandaa 'Waajiri Health Bonanza' ili kuwaweka pamoja katika michezo mbalimbali.

Katika Bonanza hilo pia alizindua Mwongozo wa VVU na Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizwa ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu,

Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu unaopaswa kutumiwa na waajiri hususani katika sekta binafsi.

Akiwasilisha salamu zake kutoka ILO, Mkurugezi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika ukanda wa Afrika Mashariki, Caroline Lugala aliwapongeza ATE kwa kuongoza vyema sekta binafsi pia kwa kuendeleza bonanza la Waajiri Afya la 2024.

"Kuandaliwa kwa bonanza la tatu la Waajiri la Afya 2024 ni uthibitisho tosha wa uwezo wa ATE kusimamia, kuendeleza na kuboresha ufanisi, uratibu na uwakilishi wa wapamoja wa sekta binafsi, ushirikiano wa afya na uzuiaji wa VVU hasa mahala pa kazi na kwenye jamii kwa ujumla" alisema 

Kwa Upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran aliwashukuru waajiri na wafanyakazi waliojitokea katika bonaza la waajiri la Afya katika viwanja vya UDSM jijini Dar es Salaam.

Bonanza hilo limeandaliwa na ATE kwa kushirikiana na shirika la Kazi duniani (ILO),OSHA, WCF, NSSSF, Helios Towers, Smiles, Dental Clinic na Shifaa hospital na kufadhiliwa na Benki ya NMB, Alaf Tanzania, DP Wold, Swissport, mcc,Stanbic bank, Cool Blue G4S na SGA.

1


2


3


3


4


5


6


7


8


9


10


11


12


13