MBIO za Shycom Alumni Marathon 2024, ambao zimeandaliwa na wanafunzi ambao waliwahi kusoma chuo cha ualimu Shinyanga (SHYCOM), ambacho zamani kilikuwa chuo cha biashara zimetamatika, huku Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akipongeza mbio hizo.
Mbio hizo zimefanyika Septemba 21,2024 katika viwanja vya michezo CCM Kambarage Manispaa ya Shinyanga, ambapo washiriki wamekimbia mbio za kilomita 5,10 na 21, pamoja na kufanyika mashindano pia kukimbiza baiskeli.
Macha akizungumza kwenye mbio hizo, amesema tukio hilo nila kihistoria ambapo wanafunzi waliowahi kusoma katika chuo hicho wameonyesha uzalendo mkubwa, kwa kuungana kwa pamoja na kuanzisha Marathon hiyo, ili kupata fedha za kuboresha miundombinu ya chuo na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya elimu na kuimarisha afya kupitia michezo.
“Tukio hili la Shycom Alumni Marathon nila kihistoria hapa Shinyanga, nawapongeza sana wanafunzi ambao mliwahidi kusoma katika chuo hiki kwa uzalendo wenu wa kukusanyika na kufanya tukio hili, ili kupata pesa za kuboresha mazingira ya chuo ambacho mlisoma na kupata elimu,”amesema Macha.
“Chuo hiki mmetoa hazina kubwa ya wasomi hapa nchini wakiwamo Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG), Profes Charles Kichere na aliyestaafu Prof Mussa Assad na leo mmpo hapa nawapongeza sana kwa uzalendo wenu na tukio kama hili, naomba liwe mfano wa kuigwa kwa watu wengine kukumbuka fadhila kwa shule na vyuo walivyosoma ikiwamo na shule ya sekondari Shinyanga (SHYBUSH) watafutane na kufanya kitu,”ameongeza.
Amesema mbio hizo pia zimesaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Shinyanga, sababu wageni kutoka maeneo mbalimbali waliwasili mkoani humo na kupata huduma mbalimbali zikiwamo za maradhi.
Jesca Domick akisoma risala kwa niaba ya wana umoja wa Shycom, amesema walikutana na kuamua kuanzisha mbio hizo za hisani Shycom Alumni Marathon, kwa lengo la kupata fedha ili kuboresha miundombinu ya chuo hicho kama kurudisha fadhila, na kwamba kila mwaka kutakuwapo na mbio hizo ikiwa na lengo pia la kuibua vipaji vya wakimbia riadha.
Mkuu wa Chuo cha Ualimu Shycom John Nandi, amepongeza mbio hizo, kwamba fedha ambazo zimepatikana zitakwenda kuboresha miundombinu ya chuo hicho, hali ambayo itasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa mafunzo.
Mmoja wa washiriki wa mbio hizo Joseph Panga, ambaye ameshinda mbio za kilomita 21,amesema mashidano hayo ni muhimu sababu yanakuza vipaji vya watu wengi pamoja na kupata ajira.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED