MACHAPISHO mbalimbali yanaeleza kuhusu Uraibu kuwa ni neno la Kiarabu ambalo kwa lugha ya kiingereza linajulikana kama “addiction” likiwa na maana ya hali inayopatikana wakati roho au mwili unahitaji mno kuwa na hisia fulani kiasi cha kuwa na matatizo katika kutekeleza shughuli mpaka kufikia tena hisia inayolengwa.
Vilevile, inaelezwa kwamba uraibu hutazamwa kama ugonjwa au utumwa wa ndani. Kwa maana rahisi ndiyo kusema uraibu ni ulevi uliopitiliza wa jambo Fulani. Mtu anakuwa hana tena uwezo wa kujizuia katika kutekeleza au kutenda jambo fulani. Hali hii ndiyo inaonekana kuikumba jami yetu katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Ni kweli kwamba uwApo wa mitandao ya kijamii umerahisisha shughuli nyingi katika jamii yetu. Kwa wale ambao tumeishi zamani kidigo kabla ya uwApo wa mitandao hii, tunaweza kukubali kwamba huko nyuma mambo mengi yalikuwa magumu katika utendaji wake japo pia kulikuwa na faida za kutokuwapo kwa mitandao hii.
Faida mojawapo ni juu ya kulinda utamaduni mzuri katika jamii zetu. Hatukuwa tunahusiana sana hasa na utamaduni wa kigeni lakini leo mwingiliano umekuwa mkubwa sana kiasi cha kushindwa kulinda utamaduni wetu.
Vilevile katika suala zima la maadili, kwa sasa kunaonekana uwapo wa mmomonyoko wa maadili kwa kiasi kikubwa. Yaani maadili yamemomonyolewa kutoka kwenye misingi mikuu na haya yamefanyika kimkakati au kwa bahati mbaya. Yako mambo hayakuwa utamaduni wetu, lakini kwa sasa yanataka kufanywa kama ya kawaida na yanapigiwa debe na wale wanaoyaamini kama utamaduni wao. Hii yote ni kutokanana na utandawazi ambao kimsingi hatuwezi kuuepuka kwa sababu dunia imeshafanywa kijiji badala yake kuwa watumiaji wazuri.
Upande wa pili, mitandao hii imerahisisha mambo mengi yakiwapo mawasiliano, maarifa mbalimbali ya kijinga na ya maana, upatikanaji wa taarifa kwa haraka, mfano zamani kuwasiliana na mtu aliyeko mkoani au nje ya nchi lilikuwa jambo gumu sana lakini sasa tunaweza kufanya vikao vya kimataifa tukiwa majumbani mwetu.
Pamoja na mafanikio hayo, kumeibuka jambo baya la matumizi ya mitandao yasiyokuwa na kiasi, yaani matumizi ya muda mrefu kwa baadhi ya watu ambalo ndilo kundi kubwa. Watu tunashinda na kulala mitandaoni huku tukidhani tumelala majumbani. Baadhi ya shughuli zinakwama au kufanyika chini ya viwango kutokana na kutumia muda mrefu sana mitandao hasa kundi la vijana. Ni jambo linaloonekana la kawaida lakini nafikiri tumefika pabaya sana.
Ukitaka kujua hili, ingia kwenye daladala au kwenye chombo chochote cha usafiri. Utaona kila mtu ameshika simu yake mkononi akiwa mtandaoni. Watu wako kiti moja lakini hawazungumzi wala kusalimiana. Unachoweza kuona tu ni kila mtu anajichekesha akiwa anafuatilia jambo fulani mtandaoni.
Yale mazungumzo ya ana kwa ana yameuawa kifo cha kawaida kabisa na hii ni mpaka nyumbani mwetu, siku hizi anakuja mgeni anakaribishwa kisha kila mmoja anashika simu yake na kuanza kujichekesha kama mtu aliyepungua mahala fulani. Wakati mwigine tunapata wageni kutoka vijijini mpaka wanajisikia vibaya na kujuta kututembelea, maana unakuta familia nzima kuanzia watoto mpaka wazazi wako mtandaoni, watoto wakiwa kwenye magemu na wazazi wakiwa kwenye tikitoku, fesibuku, twita, makundi ya wasapu na kadhalika. Huu ndio unaitwa uraibu wa kimtandao.
Kwa haraka haraka, tunadhani haya ndiyo maendeleo lakini kuna athari kubwa sana za kijamii. Hata maandiko matakatifu yamesema kuwa na kiasi kwa kila jambo. Tunapokosa kiasi tunaathirika moja kwa moja. Wengine wanaenda mbali zaidi wamefika mahali pa kujibadilisha mpaka rangi zao za ngozi ili wafanane na wale wanaowatazama kila wakati mitandaoni. Unakuta binti wa miaka 16 amejikoboa ili mradi tu apige picha aonekane mzungu mweusi. Akifikisha miaka 40 atakuwa anafananaje?
Watoto wako kwenye hatari zaidi na hapa niwaase kinamama. Simu za kinamama zinatumiwa sana na watoto wadogo kama kinga ya kuzuia wasilie kama ambavyo watani zangu kule Iringa, walivyokuwa wanatumia kilevi aina ya ulanzi kuwatuliza watoto walipokuwa katika shughuli hasa za kilimo. Matokeo yake, watoto wengi wanapokuwa watu wazima wanaingia kwenye ulevi wa pombe ndivyo itakavyotokea kwa watoto wetu. Mtoto kama anatakiwa kunyamaza anyamaze bila kutumia kitu kingine, tunadhani kwamba kwa kuwapatia simu tunaonyesha upendo wa hali ya juu mnatengeneza matatizo makubwa bila kujua.
Utasikia baadhi ya wazazi wanasema ohoo watoto wapewe tu maana ni vigumu kuzuia! Malezi gani hayo, tunataka kila anachokitaka mtoto tumpatie? Mbona hatuwapi sumu za panya maana yake tunafahamu wazi kuwa zinaua, kwa nini tusione matumizi ya simu katika umri mdogo ni hatari kama sumu ya panya?
0689157789
Dar es salaam-Tanzania
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED