MAMIA ya wananchi wa Wilaya ya Kinondoni wamejitokeza kwa wingi kupata huduma ya msaada wa kisheria bure iliyotolewa na Shirika la Citizen Foundation kwa kushirikiana na Mama Samia legal Aid Campaign katika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma jana Mkurugenzi wa Mama Samia legal Aid Campaign, Ester Msambazi, amesema wananchi wamejitokeza kwa wingi na wengine wametoka katika maeneo mengine hali inayoonesha ipo haja kwa watoa huduma za msaada wa kisheria kuwafuata wananchi badala ya kuwasubiria maofisini.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni namba moja katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria na viongozi wengine ambao ni Waziri wa Katiba na Sheria, Pindi Chana, katibu Mkuu, Mary Makondo na wadau wengine ambao ni wanawake wanaonesha juhudi za pamoja kuhakikisha kila Mwananchi anaweza kufikiwa na haki anaipata kwa wakati.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Citizen Foundation, Lilian Wassira, amesema wamezindua kliniki ya msaada wa huduma ya kisheria kwa wananchi wa Wilaya ya Kinondoni ikiwa ni mwendelezo baada ya kukamilisha katika Wilaya za Temeke na Kigamboni kwa mafanikio makubwa.
Wananchi waliojitokeza wameshukuru na kupongeza hatua ya Rais Samia kusogeza huduma ya msaada wa kisheria imekuwa msaada mkubwa hasa kwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za wanasheria.