WABUNGE wanne kati ya 17 waliolazwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) wameruhusiwa baada ya afya zao kuimarika, huku wengine wakiendelea na matibabu.
Majeruhi hao walipata ajali juzi eneo la Mbande wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakienda Mombasa, Kenya kwenye mashindano ya 14 ya Mabunge ya Afrika Mashariki.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura wa BMH, Dk. Winnie Msangi, alisema wabunge hao waliruhusiwa baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari bingwa hospitalini hapo na afya zao kuonekana kuimarika.
Dk. Msangi alisema majeruhi wengine waliosalia wanaendelea kupatiwa matibabu chini ya uangalizi wa madaktari, ili kuhakikisha afya zao zinaimarika na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Ajali hiyo ilitokea juzi na kusababisha majeruhi 23 ambao walipelekwa katika mospitali mbalimbali ikiwamo BMH kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Kamishna msaidizi Mwandamizi (SACP) George Katabazi, ajali hiyo ilitokea saa 2:00 asubuhi katika barabara kuu ya Dodoma- Morogoro eneo la Mbande, Kongwa na kusababisha majeruhi ambao ni wabunge 17, askari wawili, maofisa wa bunge wawili, dereva na kondakta.
Katabazi alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyekuwa anaendesha basi la kampuni ya Shabiby, kushindwa kuchukua tahadhari wakati akitaka kulipisha gari lililokuwa mbele yake alilotaka kulipita.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED