VIKOSI vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), vimefanikiwa kuzuia jaribio la mapinduzi lililohusisha wapiganaji wa Kongo na wa kigeni leo Jumapili asubuhi.
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi hilo, Sylvain Ekenge katika hotuba yake iliyotolewa kwa njia ya televisheni.
"Jaribio la mapinduzi limezimwa na vikosi vya ulinzi na usalama. Jaribio hilo lilijumuisha wageni na Wakongo. Wageni hawa na Wakongo wameshindwa, akiwemo kiongozi wao," amesema Ekenge.
Tina Salama ambaye ni msemaji wa Rais Felix Tshisekedi, pia amethibitisha kwa shirika la habari la Reuters kwamba Ikulu ya Rais imeshambuliwa lakini jeshi lilikuwa limechukua udhibiti.
Awali, walinzi wawili na mshambuliaji mmoja waliuawa katika shambulio dhidi ya nyumba iliyo karibu ya Vital Kamerhe, mbunge ambaye anatarajiwa kuwa spika, msemaji wa Kamerhe na balozi wa Japan wamethibitisha kupitia jumbe za mtandao wa kijamii wa X.
Ubalozi wa Marekani umetoa tahadhari ya usalama siku ya Jumapili ukionya kuhusu shughuli zinazoendelea kufanywa na maafisa wa usalama wa DRC na ripoti za milio ya risasi katika eneo hilo.
Ukurasa wa Facebook unaoonekana kuwa wa Christian Malanga, mwanasiasa anayeishi Marekani, ulichapisha video ya moja kwa moja ambayo alionekana kuongoza mashambulizi hayo.
"Sisi, wanamgambo, tumechoka. Hatuwezi kuendelea na Tshisekedi na Kamerhe, wamefanya mambo mengi ya kijinga katika nchi hii," amesema.
Tshisekedi alichaguliwa tena kwa muhula wa pili kama Rais mwezi Desemba, lakini bado hajaunda serikali, wiki sita baada ya kumteua waziri mkuu.
Kamerhe alikuwa mgombea wa Spika wa Bunge katika uchaguzi ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Jumamosi lakini ukaahirishwa na Tshisekedi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED