Simba yapigwa faini, shabiki afungiwa kuingia uwanjani

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:24 AM Mar 26 2024
Shabiki wa Klabu ya Simba aliyetambuliwa kwa jina la Mohamed Salehe akiwa ameingia uwanjani katika michezo dhidi ya Mashujaa FC.

SHABIKI wa Klabu ya Simba aliyetambuliwa kwa jina la Mohamed Salehe amefungiwa kutohudhuria mechi yoyote ile uwanjani kwa muda wa mwaka mmoja, kwa kosa la kuingia uwanjani wakati mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hiyo dhidi ya Mashujaa FC ikichezwa.

Taarifa inaeleza kuwa Bodi ya Ligi inaendelea na uchunguzi kwa lengo la kufahamu wahusika wengine wa tukio hilo ambao hawakutambulika mara moja kwa ajili ya kuchukua hatua za kikanuni.

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu.

Pamoja na hilo, Klabu ya Simba pia imepigwa faini ya Sh. milioni moja kwa kosa la walinzi wake na shabiki kupanga njama na kufanikisha azma ya kuingia uwanjani na kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina wakati wa mchezo huo, katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Taarifa imeeleza, mashabiki hao walionekana kupitia video fupi iliyosambaa mitandaoni na walijadiliana na mlinzi wa uwanjani kabla ya kuingia uwanjani na kufanya tukio hilo lililoleta taswira mbaya kwa Ligi ya Tanzania.

Bodi imesema, kwa mujibu wa kamati hiyo, adhabu hiyo ni kwa kuzingatia Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.