Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samweli Mwambugu, amesema katika kipindi cha miaka mitatu, serikali imeufungua Mkoa wa Shinyanga kwa miradi mbalimbali ya Ujenzi na ukarabati wa Miundombinu ya barabara na madaraja.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mafanikio kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya ujenzi; Mhandisi Mwambugu alisema ndani ya muda huo serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendeleza miradi mbalimbali mkoani humo.
Alisema miradi minne ya Kitaifa inaendelea kutekelezwa ikiwemo upanuzi na Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli, Ujenzi wa barabara ya Mwigumbi - Lamadi kwa kiwango cha lami, Sehemu ya kwanza Mwigumbi-Maswa ( Km50.3), Ujenzi wa barabara ya Kagongwa-Bukoba - Nzega, (km 66) ambapo Km 11.3 zipo katika Mkoa wa Shinyanga pamoja na Ujenzi wa barabara ya Kahama - Kakola (Km 73) kwa kiwango cha lami.
Alisema pia kumefanyika upembuzi yakinifu na Usanifu wa kina kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami, barabara ya Kolandoto - Laiago ( Km 53), Salawe-Old Shinyanga( Sehemu ya Solwa-Old Shinyanga, 64.66), Uyogo - Nyamilangano-Nyandekwa - Kahama, Km 54 zipo Shinyanga hadi Kaliua na Mpanda pamoja na barabara ya Old Shinyanga - Bubiki( Km 35).
Mhandisi Mwambugu aliishukuru serikali kwa kutekeleza mradi wa kusimika jumla ya taa 395 katika Miji na vijiji vya Tinde, Isaka, Kagongwa, Kahama, Segese na Bulige ikiwa ni pamoja na taa nyingine zitakazofungwa maeneo ya Vijiji vya Solwa na Ngaya.
Alieleza "Serikali imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya maendeleo na matengenezo ya barabara kwa Mkoa wa Shinyanga ili kufanya mtandao wa barabara uweze kupitika kipindi chote cha mwaka”.
Aidha Katika Miundombinu Mkoa wa Shinyanga unahudumia mtandao wa barabara zenye jumla ya Km 1,177.74 na Madaraja 309, kati ya Km 1,177.74 barabara za lami ni Km 261.102 na barabara za Changarawe ni Km 916.72.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED