KIUNGO mshambuliaji mpya wa Azam FC, Zidane Sereri, amewataka mashabiki wa klabu hiyo, kusubiria mambo mazuri kutoka kwake, pale utakapoanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Machi, mwaka huu.
Sereri alisema hayo jana, siku moja tu baada ya kutangazwa kusajiliwa na Azam FC kwa mkataba wa miaka mitano, utakaomalizika 2030.
"Nina furaha kubwa kujiunga na klabu kubwa kama Azam FC, ni moja ya klabu kubwa nchini, naamini nitakuwa kwenye wakati nzuri, nawaambia mashabiki wa timu hii wakae mkao wa kula kwani mambo mengi mazuri yanakuja," alisema mchezaji huyo ikiwa ni kauli yake ya kwanza kwa vyombo vya habari tangu atangazwe kujiunga na klabu hiyo.
Sereri amejiunga na Azam, akitoka Dodoma Jiji, ambako amecheza kwa kiwango kikubwa kwenye mzunguko wa kwanza, akiwa na mabao mawili mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Unakuwa ni usajili wa pili kufanyika kwa klabu hiyo, kwani siku chache zilizopita ili msajili beki wa kati raia wa Ivory Coast, Zouzou Landry kutoka Klabu ya AFAD Djekanou ya nchini humo.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Thabit Zacharia, amesema usajili unaofanyika ni kwa matakwa ya Kocha Mkuu, Rachid Taoussi, ambaye alihitaji marekebisho madogo kwenye kikosi chake.
Azam, tayari imeshaanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, huku kila wiki ikitarajia kucheza michezo ya kirafiki ya ndani.
"Tulianza mazoezi tangu Jumatatu ya wiki iliyopita, kujiandaa na mechi za mzunguko wa pili, tunaendelea hivi na mazoezi, lakini kila baada ya wiki moja tutakuwa tunacheza michezo ya kirafiki.
Nia ni kuangalia jinsi gani tunapiga hatua. Huwezi kufanya tu mazoezi kila siku halafu hujui umefikia wapi, ndiyo maana kocha wetu akasema kuwa anahitaji kufanya mazoezi kila siku baada ya mazoezi hadi pale Ligi Kuu itaporejea tena mwezi Machi," alisema Zakazi.
Hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, Azam ipo kwenye nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ikikusanya pointi 36, ikicheza michezo 16, kushinda 11, sare tatu, ikipoteza mechi mbili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED