Yanga yatwaa ubingwa wa 30 Tanzania Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:50 AM May 14 2024
news
Picha: Bin Zubeiry
Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize (kulia), akipongezwa na kiungo wa timu hiyo Stphane Azizi Ki, baada ya kuifungia timu hiyo bao kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar jana uwanja wa Manungu, Morogoro.

HATIMAYE mabingwa watetezi Yanga, wamefanikiwa kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo, baada ya kuitwanga Mtibwa Sugar mabao 3-1, katika mechi iliyochezwa jana jioni kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro.

Ubingwa huo unakuwa wa 30 kwa timu hiyo, tangu ilipotwaa kwa mara ya kwanza mwaka 1968, ikiwa ni mara ya tatu kutwaa mfululizo.

Ilifanya hivyo mwaka 1991, hadi 1993, ikatwaa tena mara tatu mfululizo mwaka 1996 hadi 1998, ikarudi tena msimu wa 2014/15, hadi 2016/17, na hii ni mara ya nne, kuanzia 2021/22.

Yanga walitangaza ubingwa huku ikiwa na michezo miwili mkononi baada ya kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote zikiwamo Azam FC na Simba zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu.

Timu hiyo pia ina rekodi ya kutwaa ubingwa mara tano mfululizo kuanzia mwaka 1968 hadi 1972, kama ilivyokuwa na watani zao wa jadi Simba ambao walifanya hivyo pia kuanzia mwaka 1976 hadi 1980.

Mabao mawili ya washambuliaji,  Mzambia, Kennedy Musonda, Clement Mzize aliyeingia kipindi cha pili, pamoja na bao la kujifunga la beki wa Mtibwa, Nasry Kombo, yaliifanya timu hiyo kutimiza lengo la kutwaa ubingwa kwenye mechi ya jana, hasa baada ya Simba kulazimishwa sare ya bao 1-1, Jumapili iliyopita dhidi ya Kagera Sugar na kuirahisishia Yanga kazi.

Ubingwa huo haukuja kirahisi, ilibidi wachezaji wa Yanga kupambana hasa baada ya kutanguliwa kwa bao la dakika ya 32 lililofungwa na Charles Ilamfya ambalo lilidumu mpaka mapumziko.

Ilamfya aliwashtukiza Yanga kwa kuitanguliza Mtibwa, akiunganisha krosi ya mchezaji anayeichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba, Jimson Mwanuke.

Mpira mrefu ulipigwa kutoka nyuma, ulikwenda winga ya kulia na kumkuta mchezaji huyo aliyekuwa peke yake akakimbia karibu na kibendera kabla ya kupiga krosi ya juu iliyomkuta mfungaji aliyeunganisha kwa kichwa na mpira kujaa wavuni na kuitanguliza Mtibwa.

Baada ya bao hilo, Mtibwa walionekana kurudi nyuma na kuzuia zaidi badala ya kushambulia, wakiuacha mpira kwa Yanga kwa muda mwingi wa mchezo na Yanga kuanza kuutawala mchezo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Yanga ilimtoa kipa, Diarra baada ya dakika 45 za kwanza kumalizika na kumwingiza kipa Aboutwalib Mshery kipindi cha pili ambaye alisajiliwa kutoka Mtibwa.

Musonda alifunga bao la kusawazisha, baada ya pasi safi ya mpenyezo kutoka kwa Mudathir Yahaya iliyomkuta akiwa kwenye nafasi nzuri dakika ya 62, akaukwamisha wavuni.

Dakika nne baadaye, beki Kombo aliwapa Yanga zawadi ya bao la pili, katika harakati za kutaka kuokoa, kwa kuuweka mpira wavuni akiunganisha shuti la Nickson Kibabage, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Joyce Lomalisa.

Mzize, ambaye aliingia badala ya Joseph Guede aliihakikishia Yanga ushindi na kuwa mabingwa msimu huu, alipopachika bao dakika 10 kabla ya mechi kumalizika akimalizia kwa urahisi kazi iliyofanywa na Bakari Mwamnyeto, ambaye alimlamba chenga kipa, Toba Reuben na kutoa kwa mfungaji.

Mabadiliko ya kuwaingiza, Mzize, Kibabage na Pacome Zouzoua kipindi cha pili yalionekana kuibadilisha Yanga na kufanya mashambulizi makali langoni mwa Mtibwa.

Mechi ilianza taratibu, timu zote zikifanya mashambulizi ya kushtukiza, lakini walikuwa Mtibwa waliofanya shambulizi kubwa la kwanza baada ya mshambuliaji Nassor Kapama kuachia shuti lililodakwa na Diarra.

Ilamfya alifanya jaribio la kwanza langoni mwa Yanga dakika ya 10, ambapo krosi ya Kassim Haruna ilitua kichwa kwake, lakini mpira ukatoka nje.

Shambulizi kali la Yanga langoni mwa Mtibwa lilifanywa dakika ya 22 na Maxi Nzengeli, ambaye aliambaa na mpira kwenye wingi ya kushoto akiwaacha mabeki lakini kabla hajafanya chochote, golikipa wa Mtibwa, Tona alitokea na kumnyima fursa ya kuliona lango vizuri na mpira kutoka nje.

Baada ya matokeo hayo, Mtibwa Sugar inaendelea kuburuza mkia, ikibakiwa na pointi zake 20 ambapo kipigo hicho kinaipeleka karibu kabisa na shimo ya kuangukia Ligi ya 'Champioship' msimu ujao.