Yanga yamzawadia Ramovic ushindi 6G

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:27 AM Feb 07 2025
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin
Picha: Mtandao
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin

LICHA ya kutokuwepo nchini, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, ametajwa kushiriki maandalizi ya timu hiyo iliyopata ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya KenGold FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi.

Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, aliliambia gazeti hili ushindi huo  ameupeleka kwa Ramovic, ambaye ameachana na klabu hiyo, Jumanne iliyopita na kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria.

Moallin alisema hauwezi kuutengenisha ushindi huo na Ramovic kwa sababu  walikuwa wote hadi dakika ya mwisho katika maandalizi.

"Kwanza niwapongeze wachezaji wangu wamefanya kazi kubwa sana, ushindi huu wa mabao sita naupeleka kwa kocha mwenzangu, Ramovic, huwezi kumtenganisha na mafanikio haya, tulifanya naye kazi kubwa katika maandalizi ya mchezo huu, kutengeneza mfumo na kuwasoma wapinzani wetu, kwa hiyo hizi pointi tatu na ushindi huu na yeye pia anahusika ameingia katika rekodi hii. Kwa maana hiyo namzawadia yeye," alisema Moallin.

Aliongeza matokeo ya ushindi mnono yametokana na kufanyia kazi mapungufu waliyobaini katika mechi iliyotangulia dhidi ya Kagera Sugar.

"Tulipoteza nafasi nyingi katika mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar hasa kipindi cha kwanza, tukapata bao moja tu, lakini katika mchezo huu 'tumeua' mechi mapema, tumefunga mabao manne kipindi cha kwanza, hii inaonyesha wachezaji wangu wamekifanyia kazi kile tunachowaelekeza pamoja na mapungufu yaliyojitokeza," alisema kocha huyo.

Aliongeza wataendelea kujiimarisha ili  kuhakikisha wanashinda mechi nyingine zinazofuata za ligi hiyo.

Naye Kaimu Kocha Mkuu wa KenGold, Omari Kapilima, alitaja sababu kadhaa zilizofanya kufungwa idadi hiyo ya mabao, ikiwa ni kichapo kikubwa zaidi kukipata kwa timu yao msimu huu.

"Tumefungwa mabao manne kipindi cha kwanza kwa sababu ya uzembe wa mabeki wangu, ukitizama kuna mabeki ambao niliwategemea watacheza niliowasajili dirisha dogo la usajili lakini hawapo, Steven Duah na Kelvin Yondani na wengine hawajacheza kwa sababu wana kadi za njano. Wapo pia baadhi ya wachezaji ambao vibali vyao havijakamilika, natumaini mechi inayofuata kila kitu kitakuwa tayari," alisema Kapilima.

Alisema kuwa bado hawajakata tamaa ya kubaki Ligi Kuu kwa sababu wana michezo 13 iliyobaki ambayo watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.