WAKATI ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, Klabu ya Yanga imeanza mchakato wa usajili kimya kimya kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano, huku ikitarajia kuacha wachezaji saba.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa ipo kwenye mazungumzo na wachezaji kadhaa kutoka pande mbalimbali za Afrika, lakini mazungumzo yanakwenda vizuri kwa wachezaji watano ambao kama mambo yatakwenda vizuri wanaweza kuvaa jezi ya njano na kijani msimu ujao.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, wachezaji hao ni winga hatari wa Petro de Luanda ya Angola, Deivi Miguel Vieira maarufu kama, Gilbetro, Cheick Diakite wa Real Bamako ya Mali, ambaye wakati mwingine hucheza kama straika na winga ya kushoto.
Wengine ni winga wa kulia wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Phillippe Kinzumbi, Abubeker Nassir Ahmed raia wa Ethiopia, anayeichezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini nafasi ya straika, na Ranga Chivaviro, straika wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, ambaye klabu hiyo ilimkosa dakika za mwisho msimu uliopita.
"Tunajua kuwa tutaacha baadhi ya wachezaji, maisha ya soka yanajulikana, tunaweza kuondokewa na baadhi ya wachezaji tegemeo, lakini kwa sababu uongozi ni imara, tayari umeshaanza mkakati wa kukabiliana na chochote kitakachotokea, ikitokea mchezaji akiondoka, tutatafuta mbadala wake ambaye uwezo wake ni kama aliyeondoka au zaidi,
hatusubiri hadi timu ifanye vibaya ndiyo tuanze kuona mapungufu, Yanga imeshapita huko," alisema mtoa taarifa huyo.
Mmoja wa wachezaji ambao inasemekana huenda akaondoka ni kinara wa mabao katika timu hiyo na Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ujumla, Mburkina Faso, Stephane Aziz Ki, ambaye anatakiwa na klabu mbalimbali kubwa barani Afrika, huku Mamelodi Soundowns, ndiyo inayoonekana kumtolea macho zaidi.
Pia, Yanga inatarajiwa kuacha baadhi ya wachezaji ambao watawapisha wenzao wapya watakaosajiliwa.
Chanzo kimesema kuwa, wachezaji saba ambao wanatarajia kuondoka mwishoni mwa msimu ni Mahlatsi Makudubela 'Skudu', Gift Fred, Zawadi Mauya, Bakari Mwamnyeto, Keneddy Musonda, Augutine Okra ambaye alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili na Nickson Kibabage ambaye yupo kwa mkopo akitokea Singida Fountain Gate, huku muda wake wa
mkopo ukiwa unatamatika mwishoni mwa msimu huu, akirejea kwenye klabu yake mama.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa beki huyo wa kulia anawaniwa na klabu ya Simba ambaye imeshapiga hodi Singida Fountaine Gate, ambayo inadai kuwa mchezaji huyo ana thamani ya Sh milioni 200.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED