Yanga yaanika ilipojikwaa CAF

By Adam Fungamwango ,, Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:18 AM Jan 22 2025
Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe

KLABU ya Yanga imesema imepata somo na imejifunza kitu kutokana na kutolewa kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo viongozi watakaa na kusuka mipango mipya, ili msimu ujao irejee kwa nguvu kubwa.

Akizungumza jiijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema walichojifunza ni kwamba kila siku zinavyozidi kusonga mbele inabidi nao wapige hatua zaidi na si kuwa palepale, huku michuano hiyo ikiwa migumu kila msimu.

Alisema msimu uliopita walifuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo wakiwa na pointi nane, lakini msimu huu wameshindwa wakiwa na pointi hizo.

Alisema hiyo inaonesha kila kukicha michuano hiyo inazidi kuwa migumu na inabidi kuboresha kikosi kila msimu ili kwenda na wakati.

"Funzo tulilojifunza ni kwamba kila siku zinavyozidi kusonga mbele inabidi na sisi tupige hatua zaidi, msimu uliopita tulifuzu kundi tukiwa na pointi nane, lakini msimu huu idadi hiyo hiyo ya pointi imeshindwa kutuvusha, safari hii hazikutosha, kila kukicha michuano hiyo inakuwa migumu, kuna kazi ya kufanya. Kama viongozi tutakaa na kusuka mipango vizuri ili msimu ujao turudi na nguvu kubwa," alisema Kamwe.

Aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga, kutulia na kuangalia mbele, huku wakijivunia mafanikio ya misimu mitatu ambayo wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi mara tatu baada ya zaidi ya miaka 20, moja ikiwa ni kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

"Hayakuwa matokeo mazuri kwetu, pointi nane hazikutosha kutupeleka robo fainali, haya maji yameshamwagika, yote tutakayoyazungumza, chochote tutakachokifanya kuhusu Ligi ya Mabingwa kitabakia kuwa hadithi tu, hakuna tunachoweza kukibadili kwa wakati huu.

Pamoja na hayo tunajivunia ndani ya miaka mitatu, tumecheza hatua za makundi kitu ambacho hatukuweza kukifanya kwa miaka 25, ikiwamo kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho," alisema Ofisa Habari huyo.

Jumamosi iliyopita, Yanga ililazimishwa suluhu dhidi ya MC Alger ya Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, matokeo ambayo yaliisukumiza nje ya michuano hiyo.

Alisema kikosi hicho baada ya mapumziko, kitaanza mazoezi kesho kujiandaa na mechi za Kombe la FA, pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Timu itarejea mazoezini keshokutwa (kesho), tuna mechi ya Kombe la FA dhidi ya Copco, ni mechi muhimu kwa ajili ya kurejesha furaha kwenye nyuso za mashabiki, tutarudi kwa nguvu kubwa," alisema.

Yanga pia inatarajiwa kushuka kwenye uwanja huo Februari Mosi, mwaka huu, kukipiga dhidi ya Kagera Sugar, ikiwa ni mechi ya kiporo cha raundi ya 16 ya Ligi Kuu.

Aidha, Rais wa Klabu hiyo, Hersi Said, amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa wamoja na kudumisha mshikamano licha ya kutolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, alisema uongozi wa klabu hiyo pamoja na benchi la ufundi lilifanya kila jitihada za kuhakikisha timu hiyo inafuzu hatua ya robo fainali lakini bahati haikuwa upande wao.

Alisema kuondolewa kwenye mashindano hayo kusitoe nafasi ya mashabiki kujigawa na kuiacha timu yao bali waendelee kuungana na kujipanga kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano ya kimataifa.

"Tulifanya kila liwezekanalo, lakini kama tulivyoona hatukuwa na bahati na wenzetu (MC Alger), wamepata nafasi ya kusonga mbele, nawaomba mashabiki wa Yanga kuendelea kuisapoti timu yao kwa ajili ya mashindano ya Ligi Kuu na Kombe la FA tuweze kutetea ubingwa wetu.

"Najua mashabiki wengi wameumia kuondolewa kwenye mashindano ya CAF, hili limetuuma sote, lakini ndio mpira ulivyo, kuanzia sasa tutajipanga kuhakikisha tunarejea kwa nguvu msimu ujao wa mashindano haya," alisema Hersi.