HATIMAYE, Klabu ya Yanga imetangaza kumsajili golikipa Abubakar Khomeiny, baada ya tetesi za muda mrefu, huku wakati wowote ikitarajiwa kwenda nchini Afrika Kusini kushiriki michuano ya Kombe la Toyota.
Khomeiny, aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars, anatarajiwa kwenda kuchukua nafasi ya Metacha Mnata, ambaye taarifa zinaeleza kuwa hatokuwa sehemu ya kikosi msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika.
Klabu hiyo imemtambulisha kipa huyo Mtanzania, baada ya awali kutangaza kumsajili beki wa kushoto raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Chadrack Boka kutoka FC Saint Eloi Lupopo ya nchini humo.
Beki huyo anatajwa kuja kuchukua nafasi ya Mkongomani mwenzake, Joyce Lomalisa, ambaye hatoendelea kuwapo tena kwenye kikosi hicho.
Khomeiny, anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Yanga kuelekea msimu ujao wa mashindano, akiwa ndiye Mtanzania pekee mpaka sasa.
Wengine waliosajiliwa na kutambulishwa rasmi ukimuacha Boka, ni Mzambia Clatous Chama na Prince Dube raia wa Zimbabwe.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema msimu huu hawatafanya usajili wa wachezaji wengi bali wachache, lakini ni maarufu na wenye uzoefu mkubwa katika michuano ya kimataifa.
"Tunasajili wachezaji wakubwa, maarufu kwenye maeneo ambayo tuna mapugufu, nilisema hatutasajili kwa mihemko, na tumethibitisha hilo, bado kuna wachezaji wapya ambao wataingia kwenye kikosi cha Yanga kuelekea msimu ujao," alisema.
Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa mchezaji ambaye Yanga wanaweza kumtambulisha ni Jean Baleke aliyekuwa akiichezea Simba kabla ya kutimkia Al Ittihad Tripoli ya Libya.
Wachezaji wote wa Yanga walitarajiwa kuripoti jana kwa ajili ya kuanza kambi, kabla ya kutangaziwa utaratibu mwingine.
"Kuhusu maandalizi ya msimu na kambi, wachezaji wetu wataanza kuingia Jumatatu (jana), 'pre season' tutaweka wapi? Pale pale Kigamboni, au tutasafiri? Tutakuja kuwajuza," alisema.
Wakati hayo yakiendelea klabu hiyo imealikwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya michuano ya Toyota Cup.
Taarifa iliyotolea na klabu hiyo inaeleza kuwa timu hiyo imealikwa kwenye michuano maalum ya Toyota Cup, ambapo itacheza dhidi ya wenyeji wao, Kaizer Chiefs kwenye Uwanja wa Bloemfontein, Julai 28, mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa Yanga iliialika timu hiyo katika mechi ya Kilele cha Siku ya Mwananchi, Julai 22, mwaka jana na kushinda bao 1-0, lililofungwa na Kennedy Musonda.
Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, amesema ni fahari kwao kualikwa kwenye mashindano hayo na kuahidi kwenda kutoa upinzani.
"Tumefurahi sana kupata mwaliko huu wa kushiriki michuano ya Toyota Cup 2024. Mechi hii inaendeleza uhusiano kati ya timu zetu mbili kubwa barani Afrika, ambayo ilianza mwaka jana tulipowaalika Kaizer Chiefs kushiriki maonyesho yetu, kwenye mechi ya kirafiki iitwayo Wiki ya Mwananchi.
"Tumefurahishwa na mwaliko huu na tunaahidi kutoa mechi ya ushindani ambayo itatusaidia kujiandaa na msimu mpya wa 2024/25," alisema Hersi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED