UONGOZI wa mabingwa watetezi na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga upo katika hatua za mwisho za mazungumzo kwa ajili ya kumpa mkataba mpya kiungo mshambuliaji wake, Stephanie Aziz Ki, imefahamika.
Yanga inajiandaa kumpa mkataba mpya wa miaka miwili nyota huyo ambaye amekuwa na kiwango kizuri msimu huu licha ya timu yake kuondolewa katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini.
Taarifa kutoka Yanga zinasema lengo la kumbakisha nyota huyo Jangwani ni kuhakikisha kikosi kinaendelea kuwa imara na kinatetea taji lake la Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA.
Chanzo chetu kiliongeza hatua ya kumpa mkataba mpya inatokana na baadhi ya klabu za Afrika Kusini ikiwemo Orlando Pirates kuonyesha nia ya kumhitaji mchezaji huyo.
Mamelodi Sundowns pia imetajwa kuhitaji huduma ya Aziz Ki, ambaye bao alilofungwa walipokutana na timu hiyo kwenye mechi ya marudiano lilikataliwa.
"Kuna hatua kubwa tumefikia katika mazungumzo baina ya Yanga na Aziz Ki, tunajua mchango wake ni mkubwa na ni wazi amekuwa na mwendelezo bora katika kikosi cha Yanga katika michezo ya Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika," kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliongeza tayari mwakilishi wa Orlando Pirates ameshafika nchini na kuanza mazungumzo ya awali na Aziz Ki ambaye mkataba wake wa sasa unafikia tamati ifikapo Juni, mwaka huu.
"Mchakato wa kumbakisha Aziz Ki unasimamiwa na Injinia (Rais wa Yanga, Hersi Said) mwenyewe, ameshafika mbali katika hatua za mazungumzo naye, nafasi ya kubakia Yanga ni kubwa na inaongezwa nguvu na nia ya kubakia klabuni kutoka kwa mchezaji mwenyewe," chanzo hicho kiliongezwa.
Kilisema pia Yanga haina nia ya kumuuza mchezaji huyo endapo itapokea ofa kutoka katika klabu nyingine kwa sababu haitaki kupunguza ubora wa timu yao.
“Hatujafikiria kumuuza mchezaji huyo, na suala la Aziz Ki linafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha anaendelea kusalia katika timu yetu, mazungumzo yanavyokwenda, tunaamini tutafikia makubaliano na atakubali kusaini mkataba wa miaka miwili.
Malengo yetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika michuano ya kimataifa kwa msimu ujao, baada ya msimu huu kuondolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu ujao tunahitaji kuvuka hapa,” kiliongeza chanzo chetu.
Naye Hersi alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa mchakato huo, Rais huyo alikiri Yanga iko katika mpango wa kufanya maboresho ya kuwaongeza mikataba wachezaji ambao mikataba ya sasa inaelekea mwishoni.
"Tunawapa mikataba mipya wachezaji wetu wote imara walioko ndani ya kikosi cha Yanga kwa ajili ya kuendelea nao katika msimu ujao," Hersi alisema.
Hersi aliongeza Yanga haina mpango wala mawazo ya kuuza mchezaji na wanajipanga kumalizana na baadhi ya wachezaji ambao wako mwenye mipango ya benchi la ufundi.
“Kila msimu tumekuwa na mipango yetu, msimu uliopita tulifika fainali ya Kombe la Shirikisho, msimu huu tumeondolewa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa tunaenda kujipanga kwa kuendelea kuimarisha kikosi chetu kwa ajili ya msimu ujao ili kufikia malengo yetu,” aliongeza Hersi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED