SIKU chache kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili, Klabu ya Tabora United, imefanikiwa kumsajili kiungo mkabaji raia wa Cameroon, Cedric Martial Zamba, kutoka timu ya Touarga ya Morocco.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imeeleza kuwa usajili huo ni wa kwanza kutangazwa rasmi na klabu hiyo, na umefanyika kwa mapendekezo ya Kocha Mkuu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Anicet Kiazayidi.
"Tumempata mchezaji mpya ambaye ni kiungo mkabaji raia wa Cameroon, anayekuja kusaidiana na wachezaji waliopo katika kuendeleza gurudumu la timu yetu na malengo yetu," ilieleza sehemu ya taarifa ya klabu hiyo jana.
Mbali na kiungo huyo, taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na kipa raia wa Gabon, Jean Noel Amonone, ambaye amezidakia Klabu za Amazulu ya Afrika Kusini na AS Arta Solar ya Djibouti, huku mara kwa mara akiwa anaitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo.
Wakati kipa huyo akitajwa kutua Tabora United, pia anatajwa kipa Fikirini Bakari kwenda kusaidiana naye, baada ya Klabu ya Singida Black Stars kuamua kumrejesha kipa wake, Hussein Masalanga.
Fikirini, kipa wa Singida, aliichezea Fountain Gate mechi za mzunguko wa kwanza kwa mkopo, huku Masalanga naye akiichezea Tabora United kwa mkopo.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amekiri kujereshwa kundini kwa Masalanga baada ya kuichezea Tabora United kwa mkopo wa miezi sita akieleza sababu ni kiwango bora alichokionesha mechi za mzunguko wa kwanza.
Kutokana na hali hiyo, Singida, wameamua kumpeleka Tabora United, Fikirini, kipa aliyerudishwa na Fountain Gate kwa kile kilichodaiwa kutoridhishwa na uwezo katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji uliofanyika Novemba 5, mwaka jana katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara, akiigharimu timu yake kufungwa mabao 3-1.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED