Tabora United yabaki Ligi Kuu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:34 AM Jun 17 2024
Timu ya Tabora United.
Picha: Mtandao
Timu ya Tabora United.

TIMU ya Tabora United imenusurika kushuka daraja baada ya jana kupata ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa mwisho wa kuwania kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Tabora walikuwa wanahitaji ushindi huo muhimu kuweza kubaki Ligi Kuu baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0.

Shujaa wa Tabora United alikuwa  mshambuliaji wa Kimataifa wa Angola, Patrick Lembo Aufumu aliyefunga mabao yote mawili, la kwanza kwa penaltı dakika ya 27 na bao la pili dakika ya 55 akimalizia mpira wa adhabu ndogo.

Kwa matokeo hayo, Tabora United inaitoa Biashara United kwa ushindi wa jumla wa 2-1 na kuifanya timu hiyo isalie Ligi ya 'Championship' kwa msimu ujao.

Ikumbukwe Biashara United imetoka ligi hiyo na imecheza hatua ya mtoano baada ya kuifunga Mbeya kwanza kabla ya kukutana na Tabora United iliyotoka kupoteza mbele ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa kwanza wa 'Play Off' kwa timu za Ligi Kuu.