BAADA ya droo ya makundi ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, zitakazofanyika mwakani nchini Morocco kutoka juzi, huku Tanzania ikiangukia Kundi C pamoja na Nigeria, Tunisia na Uganda, benchi la ufundi la Taifa Stars limesema halihofii hata kidogo timu walizopangwa nazo, badala yake watapambana kuhakikisha wanasonga mbele na kufuzu hatua zinazofuata.
Mmoja wa makocha wasaidizi wa Taifa Stars, Jamhuri Kihwelo 'Julio', akizungumza kutoka nchini Morocco ambako droo hiyo ilipangwa kwa timu zote 24 zilizotinga fainali hizo, alisema kinachotakiwa ni kujipanga na kuhakikisha wanachagua timu imara ya kuweza kupambana, licha ya kuwapo kwa timu kama Nigeria na Tunisia.
Licha ya Nigeria, iliyotinga fainali mwaka jana ikiwa na washambuliaji nyota kama Ademola Lookman na Victor Osimhen, Julio alisema anashangaa kuona baadhi ya mashabiki wa soka nchini kwenye mitandao ya kijamii wameanza kuwakatisha tamaa kwa kudai kundi hilo ni gumu badala ya kuwatia moyo.
"Sijaona sehemu yoyote kama kuna kundi jepesi, makundi yote ni magumu, kinachotakiwa Watanzania ni kutiana moyo, kujiandaa kwa ajili ya kupambana ili kufanya vizuri, lakini nimeanza kuona kwenye mitandao watu wakisema maneno mengi kuwa kundi ni gumu, hatuwezi, tutaenda kushiriki tu, lakini tulipofuzu fainali hizi hakuna mtu yoyote aliyetusifia," alisema kocha huyo.
Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni Watanzania kuungana na kila mmoja achukue nafasi yake ili kujiandaa na fainali hizo badala ya kutishana au kukatishana tamaa.
"Nadhani kwa hili Watanzania wote inabidi mtuunge mkono sisi watu wa benchi la ufundi na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), kwa ujumla ili tuwapambanie kwa hili ambalo limetokea, matokeo yake wameona kundi wanaona kama vile tumeshatolewa, ikumbukwe tumefuzu kwa kuifunga timu ngumu ya Guinea, sisi kama makocha chini ya Hamed Suleiman 'Morocco', tuna imani kuwa tunapambana kwa ajili ya kufanya vizuri.
"Hatuhofii timu yoyote, ukiwa katika michuano kama hii, timu kama hizo ni lazima ucheze nazo, huwezi kupewa timu mchekea zote, na sisi pia Tanzania tumeshakuwa timu kubwa sasa, tutapambana ili kuhakikisha tunafuzu," alisema Julio.
Katika droo hiyo, Ivory Coast itaanza kutetea taji lake la Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Msumbiji, huku wenyeji Morocco na waliofuzu nusu fainali Kombe la Dunia 2022, watafungua michuano hiyo dhidi ya Visiwa vya Comoro mjini Rabat Desemba 21, mwaka huu.
Michuano hiyo itaanza Desemba 21 hadi Januari 18 nchini Morocco kabla ya nchi hiyo kuandaa Kombe la Dunia la 2030 pamoja na Hispania na Ureno - timu walizoziondoa kwenye Kombe la Dunia la 2022 na kuwa taifa la kwanza la Afrika kuwahi kufika nusu fainali kabla ya kufungwa na Ufaransa.
Katika Kombe la Afrika lililopita, mwaka mmoja uliopita, Morocco ilitolewa kwa mshangao katika hatua ya 16-bora na Afrika Kusini.
Ivory Coast ilishinda Kombe hilo la Afrika kama taifa mwenyeji na wataanza kutetea ubingwa wao katika kundi moja na Cameroon, Gabon na Msumbiji.
Misri yenye nyota Mohamed Salah ambaye analitafuta taji la kwanza la Kombe la Afrika, atakuwa na umri wa miaka 33, wakati michezo inaanza Desemba, ikipangwa kundi moja na Afrika Kusini, Angola na Zimbabwe.
Senegal, bingwa wa mwaka 2021 atamenyana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Benin na Botswana wakati Algeria ipo Kundi E pamoja na Burkina Faso, Equatorial Guinea na Sudan.
Michezo itachezwa katika miji sita: Agadir, Casablanca, Fez, Marrakesh, Rabat na Tangier.
Washindi wawili wa juu katika kila kundi pamoja na washindi wanne bora waliomaliza katika nafasi ya tatu wataingia katika hatua ya 16 bora.
Droo kamili:
Kundi A: Morocco, Mali, Zambia, Comoro
Kundi B: Misri, Afrika Kusini, Angola, Zimbabwe
Kundi C: Nigeria, Tunisia, Uganda, Tanzania
Kundi D: Senegal, DR Congo, Benin, Botswana
Kundi E: Algeria, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Sudan
Kundi F: Ivory Coast, Cameroon, Gabon, Msumbiji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED