SIMBA na Yanga zote za jijini, Dar es Salaam zimekutana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jana alfajiri, kila mmoja akiwa anaelekea katika majukumu ya mechi ya mashindano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), zitakazochezwa keshokutwa katika viwanja viwili tofauti.
Simba inayoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho imeelekea mjini Luanda, Angola kuwafuata wenyeji Bravos do Maquis wakati Yanga wao wanaenda kupambana na Al Hilal ya Sudan ambayo inacheza michezo yake ya kimataifa kwenye Uwanja wa De la Capitale jijini Nouakchott, nchini Mauritania.
Akizungumza na gazeti hili muda mfupi kabla ya kuanza safari, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kwa sasa wanahitaji zaidi miguu ya wachezaji ifanye kazi kuliko maneno.
Kamwe alisema yanaweza kuzungumzwa maneno mengi, lakini ukweli kwa sasa walipofikia hawahitaji maneno zaidi ya wachezaji wao kuonesha vitendo kwa kupambana uwanjani kwa ajili ya kutafuta ushindi.
"Wachezaji wanatambua nini wanatakiwa kukifanya, nimepata bahati ya kuzungumza nao wamesema wanajua jukumu walilonalo na namna gani wanachama na mashabiki wanawategemea.
Mimi naweza kuzungumza maneno mengi, lakini ukweli tunahitaji miguu ya wachezaji zaidi na si maneno. Tunahitaji mguu wa Prince Dube, Stephane Aziz Ki, Ibrahim Hamad 'Bacca' na Dickson Job ifanye kazi tupate matokeo mazuri," alisema Kamwe.
Aliongeza katika mchezo huo wanahitaji ushindi tu kwa sababu hata matokeo ya sare hayawezi kuwasaidia, hivyo ni ushindi ndiyo utawarudisha katika matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali kutoka Kundi A.
"Hautakuwa mchezo mwepesi na sisi hatutauchukulia kiwepesi, tunafahamu tunacheza na timu ngumu, kinara kwenye kundi letu. Tuna pointi nne tunakwenda kupambana na Al Hilal, tukishinda tutakuwa tumeweka karibu zaidi matumaini yetu ya kutinga hatua ya robo fainali, si mechi ya fainali, ila itatusogeza mbele, tunajua jamaa pamoja na kwamba wamefuzu, lakini watataka kushinda ili wawe kwa kwanza.
Unapokuwa wa kwanza kwenye kundi unakuwa na faida mbili, kwanza unakutana na timu iliyomaliza nafasi ya pili kutoka kundi lingine, ya pili utaanzia ugenini na kumalizia nyumbani, hii ni faida kubwa sana katika michuano hii ya kimataifa, kwa hiyo mechi yetu pia wataitolea macho," Kamwe aliongeza.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Abdihalim Moallin, alisema uzoefu wa wachezaji wa Yanga, unawapa matumaini ya kushinda mchezo huo wa ugenini.
"Tunakwenda kusaka pointi tatu, natumaini tutazipata, wachezaji wetu hawana presha kwa sababu wameshacheza mechi nyingi kubwa, msimu uliopita walicheza michezo kama hii, wanajua jinsi gani ya kufanya. Al Hilal ni timu nzuri na hatari, lakini tumefanya kazi ya kuiangalia na kuangalia ni jinsi gani tutakwenda kucheza nao katika mechi hii," alisema Moalin.
Mechi nyingine ya Kundi A itawakutanisha MC Alger ya Algeria ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), ambayo inaburuza mkia ikiwa na pointi mbili.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema wanakwenda kucheza mchezo wa 'kimkakati' dhidi ya wenyeji Bravo do Maquis ya Angola kwa sababu hautakuwa rahisi kutokana na nafasi ya wapinzani wao.
Fadlu alisema wanakwenda kucheza mechi hiyo kwa uangalifu mkubwa kwa sababu wanahitaji kumaliza dakika 90 wakiwa wamefuzu hatua ya robo fainali.
"Itakuwa ni mechi ngumu na ya tofauti sana, tunakwenda kucheza na timu ambayo ni nzuri sana ikiwa nyumbani kwao, huwa wanamiliki sana mchezo.
Tunatakiwa kuwa makini, tunatakiwa tuwe waangalifu, tukiwa na mpira na kipindi ambacho hatuna, kwa maana hiyo tunakwenda kucheza kimkakati, nia ni moja tu tusipoteze mchezo, tushinde au tupate sare," alisema kocha huyo.
Akiichambua Bravo do Maquis, alisema ni timu ambayo ikiwa kwao imekuwa na rekodi ya kushinda mabao mengi, lakini yenyewe pia ikiruhusu nyavu zao kutukiswa, hivyo wanatakiwa kuutumia vyema udhaifu huo ili kudhibiti nguvu zao.
"Ukiangalia ni timu ambayo inafunguka ikiwa kwao, ndiyo maana inafunga mabao mengi na kuachia mianya ya wao kuruhusu, lakini sisi hatuingii katika mtego huo, hatuwezi kufunguka kama wao wanavyocheza na kupishana nao, kwa sababu hicho ndicho kilichosababisha CS Constantine ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia kufungwa mabao matatu kila moja, sisi itabidi tuwe waangalifu sana, tutapishana nao, tutawadhibiti na kutumia udhaifu wao kuwaadhibu," alisema kocha huyo.
Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema ingawa wanahitaji pointi moja ili kusonga mbele, lakini wao hawaendi kusaka sare, badala yake wanataka ushindi katika mchezo huo wa Jumapili.
"Tunakwenda kupambana kwa ajili ya kuingia robo fainali, lakini ukweli hatuendi kufanya kazi nyepesi kwa sababu mpinzani wetu naye ana nafasi, akishinda na yeye anajiweka kwenye nafasi nzuri, na mpinzani wetu anaonekana amewekeza sana kushinda nyumbani, kifupi Jumapili ni kama mechi ya fainali ya Kundi A kwenye Kombe ya Shirikisho.
Mahesabu yanaonyesha sisi tunahitaji pointi tatu au moja, na katika mpira wa miguu ni ngumu sana kuisaka pointi moja, sisi tunakwenda kusaka tatu na ikishindikana ndiyo tupate moja," Ahmed alisema.
Simba ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi lao ikiwa imezidiwa na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya vinara, CS Constantine mwenye pointi kama hizo, ambayo nayo siku hiyo hiyo, itakuwa nyumbani kucheza dhidi ya CS Sfaxien.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED