WAKATI kiungo wake, Fabrice Ngoma, akirejea nchini kuungana na wachezaji wenzake, uongozi wa Simba umesema unaendelea na mikakati ili kuhakikisha wanaiondoa Al Ahly Tripoli ya Libya katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikikisho Afrika, imeelezwa.
Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka nchini kati ya Septemba 12 au 13, mwaka huu kuelekea Libya tayari kwa mchezo huo ambao sasa utachezwa Septemba 15, mwaka huu.
Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Septemba 14, mwaka lakini sasa umesogezwa mbele kwa siku moja.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema viongozi pamoja na benchi la ufundi wanaendelea na mikakati kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zote mbili za michuano hiyo.
Ahmed alisema wameshawafahamu wapinzani wao na kwa sababu hiyo wanafahamu watakavyoingia uwanjani kuwakabili.
“Benchi la ufundi linaendelea na miakakati ya kiufundi kuhakikisha tunafanya vizuri, lakini pia viongozi kwa nafasi yao nao wanaendelea na mipango kuhakikisha timu inasonga mbele,” alisema Ahmed.
Aliongeza uongozi umejipanga kuhakikisha kila kitu ambacho benchi la ufundi wanakihitaji kuelekea katika michezo hiyo miwili kinapatikana ili timu hiyo ifanye vizuri na kusonga mbele.
Alisema ili kujiweka katika nafasi salama na kufikia malengo, Kocha Mkuu, Davids Fadlu, ameomba kupatiwa mechi nyingine ya kirafiki na tayari maombi hayo yamefanyiwa kazi.
"Mara baada ya mchezo wa kirafiki wiki iliyopita dhidi ya Al Hilal, Kocha Fadlu alisema anaomba kupata mchezo mwingine wa hiyo ya kirafiki kuelekea kwenye mchezo wa klabu bingwa Afrika inamaana kubwa kwake katika kukiandaa kikosi.
Wakati huo huo, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema maandalizi ya safari ya kuelekea Libya katika hatua za mwisho.
"Tunaendelea na maandalizi ya safari, tunatarajia kuondoka kati ya Septemba 12 au 13, hii itategemea na upatikanaji wa ndege, nchi ile kuunganisha ndege kuna changamoto kiasi fulani," alisema Rweyemamu.
Katika hatua nyingine, mechi kati ya Azam FC dhidi ya Simba imepangwa kufanyika Septemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Awali mechi hiyo ilikuwa haijapangiwa siku kutokana na kutotaka kugongana na Kalenda ya Kimataifa ya FIFA.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED