Simba yaanza safari yake kuwania taji Ligi Kuu

By Somoe Ng'itu ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:42 AM Aug 18 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davis.
Picha: Simba SC
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davis.

SAFARI ya matumaini ya wanachama, mashabiki, viongozi na wachezaji wa Simba kuurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabuni kwao baada ya kuukosa kwa misimu minne iliyopita inaanza leo watakapoikaribisha Tabora United kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davis, aliliambia gazeti hili jana anaamini timu yake itaibuka na ushindi ingawa haitakuwa mechi rahisi.

Fadlu alisema haifahamu vizuri Tabora United, lakini amekiandaa vyema kikosi chake kuibuka na ushindi katika mchezo wao huo wa kwanza msimu huu.

"Mechi za kirafiki na Ngao ya Jamii zimetujenga, lakini zimetupa somo na kujua nini cha kufanya, sasa tunakwenda katika mechi za ushindani. Hatuifahamu vizuri timu hii (Tabora United), inachezaje, lakini tunaamini maandalizi yetu yatatusaidia. Katika soka lolote linaweza kutokea, tunakwenda kucheza na timu nzuri lakini tunajiamini tutaibuka na ushindi," alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.

Naye Kocha Mkuu wa Tabora United, Francis Kimanzi, alisema wataingia katika mechi hiyo wakiiheshimu Simba kwa sababu ni moja kati ya timu kubwa si Tanzania tu, bali barani Afrika.

"Kwanza kabisa ni lazima tuwaheshimu kwa sababu ni timu kubwa, inahitaji matokeo mazuri na huwa inayapata kila mara, hii itakuwa ni kipimo kizuri kwa timu yangu ya Tabora United. Tunajua hatukuwa na wakati mzuri msimu uliopita, tunajaribu kupandisha morali ya wachezaji waliokuwepo msimu uliopita, pia watu wakumbuke sasa timu hii ina wachezaji wengine wapya na benchi jipya la ufundi," alisema Mkenya huyo.

Simba imesajili wachezaji wapya 14, tisa wa kigeni na watano wazawa, hii baada ya kupitisha 'fagio' katika kikosi chake, nyota hao wapya ni Moussa Camara, Joshua Mutale, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoa, Debora Fernandes Mavambo, Augustine Okajepha, Valentin Nouma, Karaboue Chamou, Lionel Ateba, Omari Omari, Abdulrazack Hamza, Valentino Mashaka, Kelvin Kijili na Yusuph Kagoma.

Msimu uliopita, Simba ilivuna pointi sita kwa Tabora United, ikishinda mabao 4-0 ugenini kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na kupata magoli  2-0 walipokutana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.