Simba, Azam za moto Ligi U-17

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:57 AM Apr 30 2024
Mpira ukiwa golini.
Picha: Maktaba
Mpira ukiwa golini.

TIMU za soka za vijana chini ya miaka 17 za Klabu ya Simba, Azam na JKT Tanzania zimeanza kwa kishindo ligi hiyo baada ya kushinda mechi zao mbili za mwanzo, michezo inayopigwa Uwanja wa TFF, Kigamboni, Dar es Salaam.

Juzi kwenye Uwanja wa huo, Simba iliichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0, na kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi sita, mabao sita ikiwa haijaruhusu bao lolote.

Mabao ya vijana wa Simba, yaliwekwa wavuni na Andrew Peter, Ng'ambi Sitta na Bashiru Salum.

Katika ligi hiyo inayozishirikisha timu za vijana ambazo klabu zao zipo Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Ihefu FC iliikandamiza Tabora United mabao 4-1, katika mechi iliyochezwa juzi, kwenye uwanja huo.

Mabao yote manne ya Ihefu, yalifungwa na Ramadhani Ally huku la kufutia machozi likifungwa na Nasri Abdul kwa mkwaju wa penalti.

Wakati Simba ikiongoza, timu ya Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, ikishinda mechi zote mbili ilizocheza, mabao ya kufunga sita, lakini ikiwa chini ya Simba kwa sababu imeruhusu bao moja.

JKT Tanzana inashika nafasi ya tatu, kwani nayo imeshinda mechi zote mbili ikiwa na pointi sita, lakini ina mabao manne ya kufunga.

Ihefu inashika nafasi ya nne, ikiwa na pointi nne, ikishinda mechi moja na sare moja, nafasi ya tano ikishikiliwa na TDS ambapo pia ina pointi nne, huku Geita Gold ikiwa nafasi ya sita na pointi tatu, na Yanga iko nafasi ya saba, ikiwa pia na pointi tatu.

Kama ilivyokuwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya vijana ya Mtibwa Sugar nayo inashika mkia kama kaka zao, ikiwa imecheza mechi mbili na kupoteza zote.